Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal
Malinzi, amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Young Africans
Sports Club, Yussuf Manji kutokana na kifo cha Makamu Mwenyekiti wa
zamani wa klabu hiyo, Isaac Shekiondo ‘Clinton’.
Shekiondo aliyefariki dunia juzi Novemba 20, mwaka huu kwenye
Hospitali ya Amana, Ilala jijini Dar es Salaam, alikuwa Makamu
Mwenyekiti katika Kamati ya Muda ya Young Africans chini ya Mwenyekiti
Tarimba Abbas na enzi zake Shekiondo anakumbukwa kutokana na ukarimu
wake na uwajibikaji mzuri katika klabu.
Katika salamu hizo, Rais Malinzi amesema amepokea kwa masikitiko kifo
cha Shekiondo kwa kuwa anafahamu vema utendaji wa Shekiondo wakati huo
akiwa Kiongozi wa Young Africans Sports Club. Ni mtu wa mpira wa miguu
ambaye amekuwa kwenye tasnia hii kwa muda mrefu wa maisha yake.
Kadhalika Rais Malinzi alituma salamu hizo kwa familia ya marehemu
Shekiondo, ndugu, jamaa na marafiki ambayo kwa muda walikuwa wakimuuguza
mpendwa wao na hivyo kutokana na kifo hicho, amewataka kuwa watulivu
kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao.
Msiba wa marehemu Shekiondo ulikuwa nyumbani kwake, Ilala
Mchikichini, Dar es Salaam ambako leo Novemba 22, mwaka huu umeagwa
katika Kanisa la KKKT Lutheran, Temeke Wailes kabla ya kusafirishwa
kwenda Korogwe kwa Shemsi mkoani Tanga kwa mazishi.
Bwana ametoa, bwana ametwaa. Mungu ampumzishe kwa amani marehemu Shekiondo.
No comments:
Post a Comment