CHAMA
CHA Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA),
kimeandaa kongamano maalum Oktoba 20 mwaka huu kuzungumzia kuhusiana na mifumo
ya kiuendeshaji ambayo klabu kongwe nchini za Simba na Yanga zipo mbioni
kuingia.
Kama tunavyojua klabu za Simba na Yanga, hivi sasa
zipo katika mchakato wa kubadilisha mfumo wao wa kiundeshaji, ambapo Simba
inataka kuingia utaratibu wa hisa, wakati Yanga inataka kukodishwa.
TASWA inaamini yapo mambo ambayo pengine wanachama,
mashabiki na hata wadau wa mpira wa miguu na wanamichezo kwa ujumla wanapaswa
kufahamu kwa undani zaidi kuhusiana na mifumo hiyo miwili ili kuwe na uelewa
mpana zaidi.
Ili kufanikisha mdahalo huo ambao ukumbi
utakaofanyika utatangazwa hivi karibuni, TASWA imeunda Kamati ya watu sita
kusimamia ambao ni Frank Sanga ambaye ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la
Mwananchi, Juma Pinto (Mwenyekiti TASWA) na Asha Muhaji (Mhariri wa michezo
gazeti la Rai).
Wengine ni Florian Kaijage (Mhariri Mipango Azam
TV), Amir Mhando (Mhariri gazeti la Spotileo/Katibu Mkuu TASWA) na Shija
Richard (Mhazini Mkuu TASWA).
Mapendekezo ya awali kuhusu washiriki wa kongamano
hilo inatarajiwa lihusishe wataalamu kwenye sekta ya michezo, wahariri wa
habari za michezo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ofisi ya Msajili wa Klabu
na Vyama vya Michezo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Wengine ni wanasheria, wataalamu
wa masuala ya hisa, viongozi wa klabu hizo na
baadhi ya wadau muhimu wa soka nchini, wakiwemo viongozi wa soka wa zamani
katika ngazi mbalimbali.
Hata hivyo kikao cha kamati hiyo kitakachofanyika
kesho Jumanne kitaandaa utaratibu mzima wa kongamano hilo, ikiwemo kupanga
waalikwa na namna ya uendeshaji utakavyokuwa na lengo pia liwe live (mubashara)
katika televisheni ili wadau wengi zaidi wafuatilie.
Nawasilisha,
Amir
Mhando
Katibu
Mkuu TASWA
10/10/2016
No comments:
Post a Comment