Pages

Thursday, October 6, 2016

SIMBA YAMWOMBA RADHI MAGUFULI KWA VURUGU




UONGOZI wa klabu ya Simba umemuomba radhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  John Magufuli kufutia vurugu zilizofanywa na mashabiki wake Oktoba mosi katika mchezo dhidi ya Yanga na kusababisha uharibifu wa mali ya umma kwenye mechi iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Tayari uongozi huo umemwandikia barua Waziri wa Habari Sanaa,  Utamaduni na Michezo Nape Nnauye kumuomba aenda kwa Rais kuwaombea radhi kwakua tukio hilo sio la kiungwana na limewasikitisha sana viongozi wa klabu hiyo.

Msemaji wa klabu hiyo Haji Manara alisema kuwa uongozi umesikitishwa na kitendo hicho kisicho cha kimichezo cha mashabiki wake kufanya fujo ya kuharibu miundombinu ya uwanja ikiwemo kung'oa viti ndiyo maana wakafikia hatua ya kumuomba radhi Rais .

"Tumeandika barua kwenda kwa Waziri mwenye dhamana ili akatuombee radhi kwa Rais kwakua tukio lililotokea limetukera na kutuharibia sifa nzuri tuliyonayo mbele ya Jamii, fujo sio jadi yetu," alisema Manara.
Manara alishauri kufungwe Kamera maalum (CCTV) kwa ajili ya kurekodi matukio yanayojitokeza uwanjani hapo ili kukomesha matendo hayo kwa kuwabaini mtu mmoja mmoja aliyehusika ili kupunguza mzigo kwa klabu ambazo unazipata kutokana na ujinga wa watu wachache.

"Tunashauri zifungwe Kamera za CCTV ili kuweza kuwabaini watu wanaofanya matendo kama haya. Niwahakikishie Watanzania kuwa tukio hili halitajitokeza tena kwa upande wetu kwavile kuna hatua tutazichukua kukomesha," alisema Manara.

Wakati huo huo Uongozi huo umetangaza kamati mpya ya mashindano itakayokuwa chini ya Mwenyekiti Muslay Al ruwah akiwa na Makamu wawili Hassan Hassanoo na Mohamed Nassoro ili kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri kwenye mashindano mbali mbali baada ya kushindwa kutamba kwa miaka kadhaa.

No comments:

Post a Comment