Pages

Thursday, October 6, 2016

SIMBA YAISHUKIA TFF NA BODI YA LIGI




UONGOZI wa Simba umelilalamikia Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya ligi kwa kutokuwa makini katika kupanga waamuzi wenye weledi wa sheria 17 za soka hasa kwenye mechi kubwa ya Simba na Yanga.
Akizungumza na wandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa kitengo cha mawasiliano wa Simba, Haji Manara alisema katika mchezo wa watani hao uliochezwa Oktoba Mosi, mwamuzi Martin Saanya alipewa jukumu la kuchezesha na kudai alichezesha vibaya.
"Haiwezekani mwamuzi anatoka kufungiwa mwaka mmoja na anapewa kuchezesha mechi kubwa kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, huko ni kukosekana kwa umakini kwa vyombo vinavyosimamia soka nchi hii."

"Mwamuzi alishindwa kumudu mchezo alikuwa anatoa maamuzi ambayo yalionekana dhahiri kuwa na faida upande wa pili hili ni suala ambalo linatakiwa kutazamwa kwa makini," alisema Manara.

Manara aliongeza pia kama kuna uwezekano waamuzi watakaochezesha mechi hizo watoke nje ya nchi na isiwe nchi za Afrika Mashariki na Kati ili matokeo yatokane na uhalisia kwani nao wanaweza wakawa na ushabiki wa Simba na Yanga na kusema wao Simba wanaweza kugharamia kuwalipa waamuzi kwani gharama zilizotokana na uharibifu ni kubwa kuliko kuwagharamia waamuzi toka nje.
"Sio mbaya waamuzi kutoka nje sisi tupo tayari kulipa gharama ila tukubali kurekebisha kanuni kwani ni bora kumlipa mwamuzi kutoka nje kuliko kutoa pesa za ukarabati na faini ambazo zinasababishwa na watu wachache ambazo zimekuwa nyingi kuliko gharama za kuwaleta waamuzi".
Manara alitoa mfano wa nchi ya Misri kwenye mechi ya Al Ahly na Zamalek kuwa wamuzi wanatoka nje ili kuondoa shaka ya matokeo ya mchezo na kusema ni vizuri tukaiga mfano huo.
Pia Manara amekubali faini y ash 200,000 aliyotozwa baada ya kuingia uwanjani mara tu ya mchezo kumalizika na kusema kitendo kile kilichangiwa na furaha baada ya wachezaji kusawazisha bao na pia alifanya hivyo kuwatuliza mashabiki.
Wakati huo huo Manara alisema kikosi cha timu hiyo kinatarajia kuondoka kesho kuelekea jijini Mbeya tayari kwa mchezo wao dhidi ya Mbeya City utakaochezwa Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Sokoine.

No comments:

Post a Comment