Kongamano la mabadiliko ya uendeshaji wa klabu za soka
limefanyika Jumamosi Oktoba 22, 2016 kwenye ukumbi wa Uwanja Mkuu wa Taifa, Dar
es Salaam.
Kongamano hilo lililoandaliwa na chama cha Waandishi wa Habari
za Michezo Tanzani (TASWA) lilishirikisha wadau zaidi ya 60 nchini.
Kituo cha televisheni cha Azam kilionesha live (mubashara)
kongamano hilo huku wajumbe wakikubaliana masuala kumi ya msingi.
Kwanza wajumbe walikubali kuwa kuna umuhimu wa kufanya
mabadiliko sasa kwa sababu muundo unaotumika kuendesha klabu za soka una
matatizo mengi.
Pili iliamuliwa klabu zijiandae vya kutosha kukaribisha
mabadiliko hayo ikiwa ni pamoja na kuboresha utawala bora (governance) kwenye
uendeshaji wa klabu.
Tatu mifumo yetu kama nchi inawezesha klabu kuwa na aina
nyingi za mifumo ya kiuendeshaji hivyo wanachama waelimishwe kwa kina kuhusu
mifumo hiyo ili wachague ulio bora zaidi kwa manufaa ya klabu zao.
Nne ili mabadiliko haya yafanyike kwa haki, inatakiwa wamiliki
wa timu hizi (wanachama) waelimishwe vya
kutosha juu ya thamani yao ili wajitambue. Kwamba thamani ya klabu kubwa nchini
haiwezi kulinganishwa na kiasi cha fedha kinachotolewa na wawekezaji hivyo
wanachama wasiingie kwenye mabadiliko wakiwa wanyonge kwa sababu wao ndio wana
mtaji mkubwa kuliko hela zinazoletwa kwa ajili ya uwekezaji.
Tano mabadiliko haya hayawezi kufanywa na wanachama na
wawekezaji pekee bila kuishirikisha serikali. Hivyo klabu zinapojipanga kwa
mabadiliko haya zihakikishe zinashirikisha serikali na Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF).
Sita mabadiliko haya yasifanywe kishabiki bali yafanywe
kitaalamu ili kutengeneza msingi Imara
utakaoepusha migogoro hapo baadaye.
Saba kuelekea mabadiliko haya, hasa katika kipindi hiki
ambacho uelewa wa wanachama ni mdogo, serikali inatakiwa kulinda maslahi ya
walio wengi kwa kuingilia kati pale inapoona kuna mwelekeo wa kuwa na
mabadiliko yanayominya maslahi ya walio wengi.
Nane mpira ni biashara ya kipekee ambayo mafanikio yake yanategemea
jinsi washindani wanavyoshirikiana. Hivyo kuelekea mabadiliko haya wanatakiwa
watumike wataalamu wa biashara ya mpira ili klabu zinapobadilika ziweke misingi
itakayokubaliana na biashara ya soka.
Tisa klabu zinao wajibu
wa kulinda hadhi zake (brand) kwa sababu eneo hilo ndio msingi wa biashara ya
mpira. Hivyo klabu zinapoelekea kwenye mabadiliko, lazima zizingatie hadhi zao
zinalindwaje.
Kumi Chama cha Waandishi wa Habari na Michezo kiliombwa
kufanya makongamao zaidi hasa kuhusiana na aina ya mabadiliko ambayo klabu
zinaweza kuingia kwa sababu inaonekana wanachama ambao ndio wamiliki wa klabu
hizi hawana uelewa wa kutosha hivyo inawapunguzia wigo wa kuchagua aina ya
mabadiliko.
SHIJA RICHARD
KATIBU WA SEKRETARIETI
KONGAMANO LA MABADILIKO YA UENDESHAJI WA KLABU ZA SOKA
Oktoba 24, 2016.
..................................................
TAARIFA KAMILI
UFUNGUZI
Kongamano lilifunguliwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la
Taifa (BMT), Mohammed Kiganja kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,
Utamaduni Sanaa na Michezo, Prof. Elisante
Ole Gabriel.
Kiganja aliwataka wajumbe kujadili hoja badala ya watu au
timu. Alisisitiza wajumbe wajadili mifumo na aina ya mabadiliko ambayo klabu
hizi zinaweza kuelekea.
Pia aliwataka TASWA kuhakikisha Waandishi wake wanaripoti
taarifa zenye weledi na zenye manufaa kwa familia ya wana michezo.
Aliongeza TASWA iunde kamati ya maadili kwa ajili ya
kuwawajibisha wanachama ambao wanaenda kinyume cha maadili.
WACHANGIAJI
PROFESA PROSPER NGOWI- Chuo Kikuu cha Mzumbe
Katika mada yake, Profesa anasema wanachama na wadau kwa
ujumla hawatakiwi kuogopa kufanya mabadiliko au kubadilisha namna ya kuendesha
vitu kwa sababu hilo ni jambo la kawaida.
Hata hivyo akadokeza kuwa wanachama wa Simba na Yanga
hawapaswi kuwa wanyonge kuelekea kwenye mabadiliko hayo kwa sababu mtaji wao ni
mkubwa kuliko pesa zinazoletwa na wafadhili.
"....(Wanachama) Mtaji wao mkubwa pengine sio pesa. Mtaji
wao mkubwa ni majina yaani brand ya timu hizi. Mtaji mwingine ni historia ndefu
ya timu hizi ya zaidi ya miaka 80 na ‘fan base’ kubwa sana. Pia vikombe ambazo
timu hizi zimeshida ni mtaji mkubwa sana katka meza ya majadiliano. Hii ni
mitaji ambayo thamani yake ni kubwa kuliko pesa. Kwa hiyo wenye timu hizi
hawapaswi kuwa wanyonge kifedha mbele ya wawekezaji. Thamani ya mitaji hii hasa
brand ni kubwa kuliko pesa."
Aliendelea kueleza, "Lazima waelewe kama wanakodisha timu
hizi, wanatoa na kupokea masharti gani? Hawapaswi kupokea tuu bali nao watoe
masharti. Waamue wanawakilishwa vipi katika uendeshaji wa timu hizi katika
nyanja zote? Brand ya timu hizi zinalindwa vipi? Ni muhimu pia kujua kuwa kama
mwekezaji atataka muda mrefu wa mkataba, Lazima wenye timu wawe na muda na
nafasi ya kufanya marekebisho ktk makubaliano baada ya muda fulani, mfano miaka
miwili au mitatu badala ya kusubiri hadi mwisho wa mkataba, mfano miaka
10", anasema Profesa Ngowi ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi na
biashara.
Profesa Ngowi anasisitiza kuwa kwa mtazamo wa kiuchumi na
kibiashara mabadiliko ni jambo la kawaida na halipaswi kuonekana la ajabu.
"Jambo hilo linapaswa kuwa la kawaida kwa yeyote
anayependa. Hakuna sababu ya kuogopa kufanya mabadiliko au namna ya kufanya
mambo" anasema Profesa Ngowi.
Anaendelea kueleza jambo la msingi katika mabadiliko hayo ni
pande zinazohusika hasa wanachama ambao ni wamiliki wa klabu kujua ni kipi
wanachokitaka.
"Inavyoonekana wanachotaka ni hali nzuri ya kiuchumi ya
timu zao. Sio jambo baya. Wawekezaji nao wanataka maslahi ya kiuchumi nalo sio
jambo baya hata kidogo," anasema Profesa Ngowi.
PATRIC MUSUSA - MENEJA WA MASOKO NA MIRADI KUTOKA SOKO LA HISA
DSM (DSE)
Mususa anasema klabu
zinapotaka kuelekea kwenye mabadiliko hasa kwa matarajio ya kuingia kwenye soko
la hisa, kwanza zihakikishe zinabadilisha mifumo yao iliyopo sasa ili iendane
na mahitaji ya soko la hisa.
Anasema lazima zisajiliwe kuwa kampuni na Wakala wa Usajili wa
Makampuni (BRELA) na pia ziandae taarifa za fedha.
Lazima zitatakiwa kuwa na Bodi ya Wakurugenzi (BOD)
watakaochaguliwa na wanahisa ambao ni wanachama
wamiliki wa klabu hizo.
Kila mwanahisa atastahili kupata gawio la faida pale kampuni
(klabu) yao itakapotengeneza faida na atakuwa huru kuuza hisa yake kama
anataka kuachanana na umiliki katika
klabu hiyo.
ANGETILE OSIAH, KATIBU MKUU WA ZAMANI WA TFF
Angetile anasema klabu zikihitaji kubadilisha mifumo yao
zinatakiwa kuzingatia utawala bora kwa kutofautisha majukumu sekretarieti na
taasisi nyingine zilizopo ndani ya klabu.
Anasema ulimwengu wa sasa mchezaji ni rasilimali(asset)
inayothaminishwa kwa fedha kwenye vitabu vya hesabu hivyo klabu lazima iwe na
wataalamu watakaoweza kukabiliana na changamoto hizo za utaalamu na nyinginezo.
Anasema klabu lazima ziwe na kurugenzi za uendeshaji, habari,
biashara, sheria, fedha na masoko na ziajiri wataalamu kwa ajili ya kuendesha
shughuli hizi. Kurugenzi hizo zinahitaji wataalamu kama waliopo kwenye taasisi
nyingine za serikali na makampuni binafsi.
Anaongeza kuwa uendeshaji wa klabu lazima uzingatie utawala
bora kwa kuzipa Uhuru na mipaka ya kazi taasisi au idara zote zilizopo ndani ya
klabu.
Anawakumbusha wadau kurejea azimio la Bagamoyo ambapo
Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) lilileta utaratibu wa kutoa leseni kwa
klabu zilizotimiza mashari.
Anasema masharti yanayotajwa yakiwemo kuwa na utawala bora,
timu za vijana n.k kama yatazingatiwa, klabu nitakuwa katika nafasi nzuri ya
kuchagua mfumo wa kujiendesha kama ni wa wanachama au wanahisa.
CHARLES
NDAKI, Mtaalam wa Masuala ya Masoko
Ndaki anasema jina la timu (brand) ni rasilimali muhimu inayitakiwa
kutunzwa na kuendelezwa kwa sababu ndio msingi wa biashara iliyopo katika soka.
Anasema klabu zinatakiwa kuweka mikakati ya kujipa upekee ili
kujitofautisha na wengine kwa lengo la kutumia vizuri jina lake kibiashara.
Anasema kwa kufanya hivyo klabu itakuwa na wigo mpana wa
wanachama na mashabiki (fun base) NA hivyo kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya
biashara kupitia jina la klabu.
MICHAEL WAMBURA - KATIBU WA ZAMANI WA TFF
Wambura anasema serikali ndio inayoweza kulinda maslahi ya
wengi katika mabadiliko haya hivyo watumie vyombo vyake kuhakikisha yanafanyika
mabadiliko yenye maslahi kwa walio wengi.
Anasema ni vyema mabadiliko yakafanyika kwa kuzingatia Sheria
za nchi, TFF, CAF na FIFA hivyo aliviomba vyombo vinavyohusika, TFF, BMT na
Wizara kuhakikisha zinawezesha mabadiliko haya kwa manufaa ya klabu, wanachama,
wawekezaji na sekta ya michezo kwa ujumla.
HENRY
TANDAU MKUFUNZI WA FIFA
Anasema wadau katika mabadiliko haya lazima wajifunze mifumo
minne ya kuendesha soka kablaya kuelekea mabadiliko.
Anaongeza tatizo kubwa la wadau wa michezo hawapendo kujifunza
wanaendesha klabu kwa mazoea.
Anasema biashara ya mpira ni ya aina yake kwa sababu ili
ufanikiwe inahitaji ushirikoane na mshindani wako. Kutokana na upekee huo,
biashara hii inatakiwa kuendeshwa na wataalamu wenye weledi nayo.
Anasema Azimio la Bagamoyo ndio lilitakiwa kuwa msingi mkubwa
wa mabadiliko kwa sababu limeanisha vitu vingi vizuri ambavyo havijafanyiwa
kazi.
Anaongeza kuwa japo tumechelewa lakini tulipofika tungeanza na
Azimio la Bagamoyo kuelekea kwenye mabadiliko ya kweli.
JAMAL
RWAMBOW, MJUMBE WA BARAZA LA MICHEZO LA TAIFA (BMT)
Anasema mabadiliko haya hawawezi kufanyika bila kuishirikisha
serikali. "Itakuwa ni kujidanganya kuamini kwamba wawekezaji na wanachama
wanaweza kufanya mabadiliko haya bila kuishirikosha serikali kwa sababu serikali
ndio baba" anasema Rwambow.
Alitoa mwito kwa wadau kuishirikisha serikali na hasa kufuata
maelekezo yaliyotolewa na BMT kuhusiana na utaratibu wa kufanya mabadiliko hayo
kama klabu zi nataka kuelekea huko.
Mwishowe Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando aliahidi kwamba
chama chake kitashirkiana wadau mbali mbali kuhakikisha makongamano kama hayo
yanafanyika Mara kwa mara ili kutoa fursa kwa wadau ya kujifunza.
No comments:
Post a Comment