TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Elisante Ole Gabriel anatarajiwa kufungua
kongamano kuhusu mabadiliko ya mifumo ya uendeshaji katika klabu za soka
nchini.
Kongamano hilo linatarajiwa
kufanyika Jumamosi Oktoba 22, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuhusu mifumo ya kiuendeshaji ambayo klabu kongwe
nchini za Simba na Yanga zipo mbioni kuingia na limeandaliwa na Chama cha
Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA).
Kongamano hilo litaanza saa nne na
nusu asubuhi na litarushwa live (mubashara) na kituo cha televisheni cha Azam
kupitia chaneli yake ya Azam Two.
Dhamira kubwa ya kongamano hilo ni
kupata maoni ya kitaalamu kuhusu mifumo hiyo, ambapo Simba ipo mbioni kuingia
mambo ya hisa, wakati Yanga utaratibu wa kukodishwa.
Baadhi ya mambo yatakayojadiliwa ni
namna ya kuendesha klabu za soka kibiashara, uwekezaji, mambo ya hisa na
masuala ya uthamini kukiwa na watalaamu kutoka taasisi mbalimbali nchini.
Pia kutazungumzwa umuhimu wa
mabadiliko katika klabu hizo na harakati za kuzibadili zilivyoanza miaka ya
nyuma na matokeo yake yalivyokuwa.
Lengo ni kujadili kitaalamu bila
ushabiki wa namna yoyote kwani nia ni kujenga na kuimarisha soka na michezo kwa
ujumla hapa nchini na ndiyo sababu tumealika wataalamu wa kada mbalimbali,
viongozi wa zamani wa soka kwa tofauti na baadhi ya wadau wa soka.
Nawasilisha,
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
21/10/2016
No comments:
Post a Comment