Pages

Tuesday, September 20, 2016

KILIMANJARO QUEENS UWANJANI LEO, JE ITALETA KOMBE NYUMBANI?



TIMU ya taifa ya Tanzania Bara ya wanawake, Kilimanjaro Queens leo inashuka dimbani kwenye Uwanja wa Ufundi, Njeru mjini Jinja, Uganda kumenyana na Kenya kwenye mchezo wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge.
Kocha wa Kilimanjaro Queens, Sebastian Nkoma amesema kwamba anatarajia mchezo mgumu kwa sababu Kenya ni timu nzuri na imefuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake, ikiwa timu pekee katika ukanda wa CECAFA lakini  wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kurejea na Kombe Dar es Salaam.
“Tunataka kuweka rekodi ya kuwa mabingwa wa kwanza wa Chalenji ya wanawake, japokuwa tunacheza na timu ngumu, Kenya. Tunajipanga kikamilifu kuhakikisha tunafanikisha hilo,”alisema kocha Nkoma
Ikumbukwe, Kilimanjaro Queens iliingia fainali baada ya ushindi wa 4-1 dhidi ya wenyeji, Uganda, wakati Kenya iliifunga 3-2 Ethiopia. Awali, Tanzania Bara iliongoza Kundi B baada ya kushinda kura ya sarafu kufuatia sare ya 0-0 na Ethiopia katika mchezo wa mwisho wa kundi hilo, hivyo kufungana nayo kwa pointi na wastani wa mabao kileleni. 
 Kilimanjaro Queens ilianza vizuri michuano hiyo kwa kuibamiza 3-2 Rwanda, mabao yake yakifungwa na Asha Rashid ‘Mwalala’ dakika za 11 na 65 na Stumai Abdallah dakika ya 28, wakati ya wapinzani wao yalifungwa na Ibangarrue Marie na Amina Ally wa Tanzania Bara aliyejifunga.

No comments:

Post a Comment