Kocha Mkuu wa timu ya soka ya
Tanzania, Charles Boniface Mkwasa amesema kwamba mchezo ujao kati ya Mapharao
wa Misri na Taifa Stars, utakuwa ni fainali ya kuamua taifa litakalofuzu katika
fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON hapo mwakani kutoka kundi G.
Akizungumza na waandishi wa
habari mara baada ya mchezo kati ya Harambee Stars ya Kenya na Taifa Stars ya
Tanzania Mei 29, 2016, uliofanyika Uwanja wa Moi Kasarani, Mkwasa maarufu kama
Master anasema kwa msimamo na hali ilivyo kwa sasa, “Najua Misri
wanatufuatilia. Na hata Kenya kwa siku zote tatu walikuwako. Najua Misri
wanahitaji sare ili wafuzu kwa fainali hizi, lakini hawataipata Tanzania.”
Mkwasa anasema mchezo dhidi ya
Misri, ana uhakika vijana wake watajitahidi ili kupata matokeo mazuri baada ya
Jumapili kufanya vema dhidi ya Harambee Stars waliocheza mechi hiyo mbele ya
mashabiki wao wachache ambao pia hawakuchangamka kama wale wa Tanzania ambao
licha ya kuwa ugenini walichangamsha mji na uwanja.
Wakati Misri wana pointi saba, Taifa
Stars ina pointi moja na hivyo wa kuibania au kupindua matokeo ya Misri isiende
AFCON mwakani, basi ni Tanzania hasa kama itawafunga Mapharao Jumamosi kabla ya
kwenda Nigeria Septemba, mwaka huu kucheza na Nigeria.
“Kama nilivyosema, Misri wanakuja
wanahitaji pointi moja lakini sisi tunahitaji pointi tatu. Mchezo wa leo
unatosha kuona mapungufu (upungufu). Maana ilikuwa mechi ngumu iliuyojaa nyota
wote wa Kenya ambao ni professionals, lakini mimi nilikuwa na local based
players na matokeo yamekuwa hayo.
“Tilianza kufunga bao, lakini
wakarudisha. Bora mchezo umeishia hivi maana najua Wakenya hawana uvumilivu,
tungewafunga hapa sijui kama tungetoka salama,” amesema Mkwasa ambaye baadhi ya
waandishi, hususani wale wa Kenya walianguka kicheko kuashiria kuwa kuna
matatizo katika utawala wa soka.
Mkwasa anasema ana taarifa namna
ambavyo Misri wanaifuatilia Taifa Star hususani ukusanyaji wa video kwa ajili
ya kuona aina ya soka la Tanzania, huku akisema: “Hawatafanikiwa kwa sababu
soccer is the game of different approach (Soka ni mchezo wenye mifumo tofauti).
Hivyo tulivyocheza na Kenya sivyo nitakavyocheza na Misri, nitakuwa na approach
yake.”
Anasema ushindi wa Jumamosi ijayo ni
wa kuvuna pointi tatu ili kupata kasi ya kushinda mchezo dhidi ya Nigeria na
kufungua ukurasa mpya wa Taifa Stars kutengeneza mazingira mazuri ya kuwashinda
Nigeria katika mchezo wa mwisho hatua ya makundi utakaofanyika Septemba, mwaka
huu.
“Tunaomba Wakenya mtuombee. Nasi
tunawaombea ili kama wote inatokea mwaka huu tunakosa mafasi, basi iwe kheri
kwa kipindi kijacho. Sisi tumekuja kucheza kwenu katika mji wenu wenye baridi
basi nanyi karibuni siku moja dar es Salaam, Tanzania katika mji wetu wetu
wenye joto, huenda mkaambulia sare vile vile,” anasema.
Mkwasa alipongeza Shirikisho la Soka
Tanzania (FKF), kwa kuandaa mchezo huo angalau kwa asilimia 70 kwa kushirikiana
na Tanzania iliyojazia gharama za juu sambamba vijana wake kwa kucheza kwa
kujituma licha ya kuwakosa nyota wake wa kulipwa na hivyo kupata picha na mbinu
sahihi za kuivaa Misri Jumamosi ijayo.
“Bado tunaendele kujenga timu yetu,
wengi ni vijana kama mlivyoona na wengine ni mara ya kwanza wanacheza. Nimewapa
nafasi na mmeona uwezo wao, bila shaka tutafanya vema maana wengine ni under 21
wako kwenye kikosi. Huko mbele tutakuwa na timu nzuri,” anasema Mkwasa
akimtolea mfano Shiza Ramadhani ambaye alipewa nafasi kwa mara ya kanza katika
kikosi cha kwanza akichukua winga ya kulia.
VICTOR WANYAMA
“Kwa hiyo tayari tumeona kitu gani
cha kuongeza,” anasema Mkwasa hoja yake iliyoungwa mkono na Nahodha wa Harambee
Stars, Victor Wanyama ambaye kwa dakika chache, alizungumza na Ofisa Habari na
Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania na kuhoji: “Unasema leo hamkuwa na
professional pale uwanjani?” alipohakikishiwa ukweli huo, akasema:
“Basi mna kikosi kizuri. Wengi ni
vijana, wanaweza kama mkicheza kwa kutubana kama mlivyobana hapa, Misri
mnaifunga na hata hao Nigeria, si ajabu nikasikia mnakwenda AFCON mwakani.
Ninaitakia kila la kheri timu hii, nawatakiwa kila la kheri Watanzania katika
harakati zao. Sisi mwaka huu tumepotea kabisa, hatuna matumaini tena,
tunajipanga ndiyo maana nimekuja kutetea taifa langu, hata kama tumekosa
nafasi,” alisema Wanyama anayekipiga Southampton ya England.
Katika mchezo huo, Taifa Stars
iliwakosa nyota wake Mbwana Samatta anayechezea Genk ya Ubelgiji kwa kuwa
alikuwa na mchezo muhimu wa kupa nafasi timu yake ama icheze Ligi ya Uropa au
ibaki nje katika michezo ya kimataifa ngazi ya klabu Ulaya. Shirikisho la Soka
Tanzania na Kocha Mkwasa walimruhusu kama ilivyo kwa Thomas Ulimwengu
anayekipiga TP Mazembe waliokuwa na mchezo mkali dhidi ya AS Vita ambao wana
utani na ushindani mkali wa soka huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
MWINYI KAZI MOTO
Naye Nahodha wa Taifa Stars katika
mchezo huo, Mwinyi Kazimoto amesema kwamba mchezo dhidi ya Kenya, umeonesha
picha ya kinachotakiwa kufanyika katika michezo ijayo inayoikabili timu hiyo
baada ya kusifu maandalizi, mapokezi mazuri na sapoti nzuri kutoka kwa
mashabiki wa Kitanzania, hasa wale waliosafiri umbali mrefu kutoka Dar es
Salaam kwenda Nairobi, Kenya kuishangilia Stars. Nahodha wa Taifa Stars ni
Mbwana Samatta anayesaidiwa na John Bocco ambao katika mchezo huo, hawakucheza.
Bocco ni Majeruhi.
MCHEZO WA HARAMBEE STARS,
TAIFA STARS
Katika mchezo huo, kipindi cha
kwanza mashabiki walishuhudia mabao 1-1 kwa kila upande na ndiyo yaliyokuwa
matokeo ya mwisho katika dakika 90, lakini kipindi cha pili wadau wa soka
walishuhudia mabadiliko ya kila timu kujaribu nyota wake kwa mujibu wa sheria
na taratibu za Shirikisho la soka la Kimataifa (FIFA), linaloruhusu kubadili
wachezaji hadi wachezaji sita. Lakini hakukuwa na mabadiliko ya matokeo.
Kuhusu mabao ni Elias Maguli ndiye
aliyetangulia kuifungia Taifa Stars bao katika dakika ya 30 kwa kichwa baada ya
kupokea krosi murua kutoka kwa Juma Abdul kutoka Mashariki ya Uwanja wa Moi
Kasarani kabla ya dakika saba baadaye kumfanyia madhambi Winga Ayub Masika
ndani ya eneo la hatari hivyo Mwamuzi, Brian Nsubuga kutoka Uganda, kuamuru
penalti iliyokwamishwa wavuni na Victor Wanyama.
Katika mchezo huo ambao wakati wote
ulikuwa ni wa kushambuliana kwa timu zote mbili, Taifa Stars iliwapumzisha kipa
Deogratius Munishi na nafasi yake ikachukuliwa na Aishi Manula na kwa wakati
mmoja kuwatoa Jonas Mkude na Shiza Ramadhani na nafasi zao kuchukuliwa na Farid
Mussa na Mohammed Ibrahim baadaye Kocha Mkwasa alimwingiza Jeremiah Juma
kuchukua nafasi ya Maguli.
Kenya wao waliwatoa Humphrey Ochieng
kwa kuingia Cliford Miheso; akatolewa tena Jesse Were kwa Wyclif Ochomo; Ayub
Masika akapumzishwa na John Makwata akapewa nafasi kama alivyopumzishwa Anthony
Agay na nafasi yake kuchukuliwa na Mayeko Mohammed. Pamoja na mabadiliko hayo,
matokeo yalibaki vilevile 1-1 hadi dakika ya 90 katika mchezo ambao Wanyama
alipewa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi Kazimoto.
VIKOSI VYA TIMU ZOTE
Vikosi vya kwanza katika mchezo,
Kenya: 1. Boniface Oluoch, 9. Joakins Otieno Atudo, 5. Abud Omar Khamis, 12.
Eugene Ambuchi Asike, 8. David Owino Odhiambo, 14. Anthony Akumu Agay, 15.
Victor Mugubi Wanyama, 23. Ayub Timbe Masika, 19. Humphrey Mieno Ochieng’ 16.
Eric Johanna Omondi, 29. Jesse Jackson Were
Wachezaji wa akiba: 3. David Okello
Abongo, 10. Eric Ouma Otieno, 6. Mayeko Musa Mohammed, 24. Victor Ali Abondo,
27, Wycliff Okello Ochomo, 20. John Mark Makwata, 21. Clifford Miheso Ayisi
Tanzania XI: 1. Deo Munishi,
6. Juma Abdul Jafari, 2. Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, 13. Aggrey Morris, 15.
Erasto Edward Nyoni, 17. Jonas Gellard Mkude, 7. Himid Mao Mkami, 16. Shiza
Ramadhan Yahya, 12. Mwinyi Kazimoto Mwitula, 10. Elias Mrugao Maguli, 4. Deus
David Kaseke
Wachezaji wa akiba walikuwa: 18.
Aishi Salum Manula, 5. David John Mwantika, 9. Farid Mussa Shah, 11. Jeremiah Juma Ally, 8. Abrahim Hajibu
Migomba, 3. Mwinyi Haji Mngwali, 14. Mohammed Ally Ibrahim
WAAMUZI
Brian Nsubuga (Mwamuzi wa kati),
Hussein Bugembe (Msaidizi wa Kwanza), Ronald Katenya (Msaidizi wa Pili), Amir
Abdi Hassan (Kamishna wa mchezo) and Davies Omweno (Mwamuzi wa Akiba,
Mezani.)
No comments:
Post a Comment