Pages

Wednesday, February 10, 2016

YANGA KUONDOKA IJUMAA KWA NDEGE YA KUKODI KUHOFIA HUJUMA






MCHECHETO wa mechi ya Ligi Kuu kati ya watani wa jadi Simba na Yanga umeifanya Yanga kukodi ndege maalumu kwa ajili kwenda Mauritius kwenye  mchezo wa kwanza wa raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Cercle de Joachim. 

Akizungumza na wandishi wa Habari jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro alisema wameamua kukodi ndege maalum ambapo sasa wataondoka Ijumaa kwenda Mauritius badala ya jana kama ilivyoripotiwa awali.

“Shirika la Ndege la Afrika Kusini  limeshindwa kutupatia ndege ya kuunganisha mapema mjini Johannesburg, kwenda Curepipe, Mauritius badala yake timu ingelazimika kusubiri kwa saa saba na wakati wa kurudi badala ya kufika Jumapili tungefika Jumatatu jambo ambalo lingefanya timu ikose siku tano za kujiandaa na michezo mitatu ambayoinatukabili mmojawapo ni wa Simba,”alisema Muro

Pia Muro alikiri kukodi ndege binafsi ni gharama lakini wamelazimika kufanya hivyo ili kukwepa hujuma ambazo wameona dalili zake na kumpa muda kocha kuendelea na programu yake kiufasaha na kuepuka uchvu kwa wachezaji.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Jumamosi  saa 9:30 Alasiri  katika Uwanja wa Curepipe na baada ya mchezo huo timu itaondoka kurudi na itafikia kambini Kisiwani Pemba na Jumapili itaanza mazoezi.

“Kocha ameendelea na programu yake leo na kesho (jana na leo) na Ijumaa wataondoka na watafikia kwenye kambi maalum ambayo tumeandaa ikiwa na wapishi wetu na baada ya mechi watapanda ndege kwani itakuwa inawasubiri tayari kurudi na watafikia kambini Pemba,” alisema Muro
Muro amesema Yanga wanakabiliwa na mchezo dhidi yao na Yanga, Mtibwa Sugar na Azam FC hivyo wanatakiwa kujiandaa vya kutosha kwani michezo muhimu na ligi imekuwa na ushindani.

Wachezaji Benedicto Tinocco ambaye ni kipa namba tatu na  mshambuliaji Matheo Anthony na kiugo Godfrey Mwashiuya wanakosa safari hiyo kutokana na sababu mbalimbali lakini Mwashiuya hana pasi ya kusafiria.
Wachezaji waliokuwa majeruhi, Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Amissi Tambwe wote watasafiri na timu na mkuu wa msafara ni Ayoub Nyenzi, ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)

Kikosi kinachokwenda Mauritus ni  Makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’ na Deogratius Munishi ‘Dida’.
Mabeki ni Juma Abdul, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Vincent Bossou na Pato Ngonyani.
Viungo ni Said Juma ‘Makapu’, Salum Telela, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Simon Msuva, Issoufou Boubacar  na Deus Kaseke.
Washambuliaji ni Malimi Busungu, Paul Nonga, Amissi Tambwe  na Donald Ngoma.

No comments:

Post a Comment