Kocha wa Simba, Jackson Mayanja akisalimiana na kocha wa Mtibwa, Mecky Mexime |
SIMBA
imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo
uliochezwa katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam leo.
Pamoja na
ushindi huo Simba imebaki kwenye nafasi ya tatu baada ya kufikisha pointi 30
sawa na Yanga inayoshika nafasi ya pili, lakini Yanga ikiwa mbele kutokana na
kuwa na mabao mengi ya kufunga.
Hiyo ni mara
ya pili kwa Simba na Mtibwa kukutana katika kipindi cha wiki mbili kwani
walikutana kwenye mchezo wa nusu fainali wa kombe la Mapinduzi na Mtibwa Sugar
kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Kwenye
mchezo wa leo Simba ilikuwa bila ya kocha wake mkuu Dylan Kerr
aliyefungashiwa virago kufuatia mwenendo mbaya wa timu hiyo, walipata bao lao
mapema kipindi cha kwanza kupitia kwa
mshambuliaji Hamisi Kiiza dakika ya nne.
Dakika ya 13 kiungo Justice Majavi alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumfanyia rafu kiungo wa Mtibwa Shiza Kichuya na dakika tatu baadae Kiiza alipoteza
nafasi nzuri ya kufunga kwa shuti lake kupaa juu ya lango la Mtibwa.
Kwenye
dakika ya 31 Simba walifanya mabadiliko kwa kumpumzisha winga Peter Mwalyanzi
na kumuingiza Said Ndemla aliyechangamsha zaidi sehemu ya kiungo ya timu hiyo.
Dakika ya 47
Mtibwa Sugar walipoteza nafasi nzuri ya kusawazisha lakini kiungo wake aliye
kwenye kiwango bora Shiza Kichuya alipiga mpira uliotoka pembeni ya lango la
Simba.
Mtibwa Sugar
walitawala kiasi sehemu ya kiungo na nusura wapate bao lakini shuti la beki wa
kushoto wa timu hiyo Issa Rashidi kwenye
dakika ya 54 kugonga mwamba na kuokolewa na mabeki wa Simba.
Timu zote
zilifanya mabadiliko kwa Mtibwa Sugar kumpumzisha Mohamedi Ibrahim na
kumuingiza Vicent Barnabas na Simba kumtoa Ibrahim Ajib aliyeumia na kumuingiza
Danny Lyanga na kipa wa Simba Vicent Angban alionyeshwa kadi ya njano kwa
kupoteza muda.
KWENYE VIWANJA VINGINE MATOKEO NI KAMA IFUATAVYO
JKT Ruvu | 1 - 5 | Mgambo JKT | |
Toto Africans | 0 - 1 | Tanzania Prisons | |
Simba SC | 1 - 0 | Mtibwa Sugar | |
Stand United | 1 - 0 | Kagera Sugar | |
Mbeya City | 1 - 0 | Mwadui FC | |
Coastal Union | 1 - 1 | Majimaji |
No comments:
Post a Comment