Pages

Tuesday, November 10, 2015

KLABU YA REAL SOCIEDAD YAFUNGASHIWA VIRAGO DAVID MOYES


David Moyes ametimuliwa kazi kama Meneja wa Klabu ya La Liga inayosuasua ya Real Sociedad ikiwa ni Siku 1 tu kabla hajatimiza Mwaka mmoja Klabuni hapo.
Moyes, mwenye Miaka 52, alitwaa wadhifa wa Umeneja wa Klabu hiyo ya Spain hapo Tarehe 10 Novemba 2014 na kuiokoa Klabu hiyo kuporomoka wakati ikiwa katika hali mbaya na kukamata Nafasi ya 12 kwenye La Liga Msimu uliopita.

Lakini Msimu huu mambo ni yale yale kwa Real Sociedad baada ya Ijumaa kuchapwa 2-0 na Las Palmas ikiwa ni kipigo cha 4 katika Mechi zao 5 zilizokwisha za La Liga.
Real Sociedad imetangaza Moyes na Msaidizi wake, Billy McKinlay, wote wamefukuzwa.
Kuhamia kwa Moyes huko Sociedad Mwaka Jana ilikuwa ni kibarua chake cha kwanza tangu atimuliwe Man United Mwezi Aprili 2014 baada ya kudumu Miezi 10 tu hapo Old Trafford.

Moyes, ambae kabla ya kutua Man United alikuwa Meneja wa Everton kwa Miaka 11, alikuwa ni Meneja wa 4 kutoka Uingereza katika Historia ya Real Sociedad.
Wengine waliomtangulia Klabuni hapo ni Harry Lowe alieingia Mwaka 1930 na kukaa Miaka 5, John Toshack alieiongoza Klabu hiyo kwa vipindi vitatu tofauti na cha mwisho kilikuwa Mwaka 2002 wakati Chris Coleman alikaa kwa Miezi 7 baada ya kuteuliwa Julai 2007.
Real Sociedad, ambao wako Nafasi ya 17 katika La Liga, watapambana na Sevilla, Mabingwa wa UEFA EUROPA LIGI, na kisha Barcelona, Mabingwa Watetezi wa La Liga na pia UEFA CHAMPIONS LIGI, katika Mechi zao 2 za La Liga zifuatazo mara baada ya La Liga kurejea tena Wikiendi ya Novemba 21 baada kupisha Mechi za Kimataifa.

No comments:

Post a Comment