Pages

Friday, September 18, 2015

YANGA KUENDELEA KUIPOTEZA JKT?




MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga, kesho wanashuka tena kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kucheza na JKT Ruvu.
Yanga inashuka dimbani ikiwa inaongoza katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kushinda mechi zake mbili na kujikusanyia pointi zote sita huku ikifunga mabao matano.
Katika mchezo wa kwanza, Yanga ilishinda Wagosi wa Kaya Coastal Union kwa mabao 2-0 kabla ya kuibuka na ushindi mwingine wa mabao 3-0 dhidi ya Prisons ya Mbeya.
Timu hiyo itacheza mechi nne mfululizo kwenye uwanja wake wa nyumbani kwani baada ya mchezo wa leo, itashuka tena dimbani kumenyana na watani zao wa jadi Simba Septemba 26 kabla ya kuanza kutoka wakati itakapocheza na Mtibwa Sugar Septemba 30 kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Yanga inahitaji ushindi katika mchezo huo ili iweze kuzidi kukalia kiti hicho na kufanya biashara mapema kabla ya kuhesabu mapato jioni.
Yanga imeshafunga mabao matano katika mechi mbili na haijafungwa bao hata moja, hivyo inaonesha jinsi safu yake ya ushambuliaji kama akina Donald Ngoma, Hamisi Msuva, Amiss Tambwe na wengineo ilivyo na uchu wa mabao, hivyo mabeki wa maafande wa JKT Ruvu watakuwa na kibarua kigumu cha kuwazuia wasifunge.
Hata hivyo, kikosi cha JKT Ruvu kinachofundishwa na mchezaji na kocha wa zamani wa Yanga, Fred Minziro hakitakubali kufa kikondoo, kwani kinazihitaji sana pointi hizo tatu ili kurejesha matumaini ya kufanya vizuri.
JKT Ruvu ndio inaburuza mkia baada ya kufungwa mechi zote mbili za mwanzo na kuifanya kuwa na kazi kubwa ya kufanya ili kutoka na pointi zote tatu au moja kwa kutoka sare.
Kocha wa JKT Ruvu, Minziro alikiri kuanza vibaya kwa ligi hiyo lakini alisema leo hawatakubali kufungwa licha ya uimara wa Yanga ambayo ina wachezaji wengi wazuri, wakiwemo wa kutoka nje ya nchi.
Alisema kuwa timu yao ilianza vibaya mechi mbili za mwanzo baada ya wachezaji wake kutokuwepo katika maandalizi ya mwisho baada ya kuwa katika mashindano ya majeshi nchini Uganda kwa takribani siku 11.
Pia alisema timu yake ina majeruhi wawili, lakini alikuwa na imani siku zinavyokwenda timu hiyo itazidi kuimarika na kufanya vizuri katika mechi zao zijazo.
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub alisema kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaondoka na pointi zote tatu ili kuzidi kungara katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 16.
Mechi zingine leo ni Stand United watachea na African Sports katika mchezo utakaofanyika kwenye uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, huku Mgambo Shooting itawakaribisha wana Lizombe Maji Maji ya Songea katika uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Mbeya City wenyewe watakuwa wageni wa ndugu zao wa Tanzania Prisons katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Wakati Mbeya City ni ya nane baada ya kuwa na pointi tatu kutoka katika mechi mbili walizocheza, Tanzania Prisons wenyewe ni wa pili kutoka mkiani wakiwa hawana pointi hata moja baada ya kuchapwa mechi zote mbili za mwanzo.
Mechi hizo zitaendelea tena kesho Jumapili kwa Mwadui ya Shinyanga kuikaribisha Azam FC huku kocha wa wenyeji hao Jamhuri Kihwelu kutamba kuibuka na ushindi.
Mtibwa Sugar watacheza na Ndanda FC katika mchezo utakaofanyika kwenye uwanja wa Manungu, Turiani wakati Simba baada ya kuanza kwa kucheza mechi mbili ugenini, kesho kwa mara ya kwanza itakuwa kwenye Uwanja wa Taifa ikicheza na Kagera Sugar.
African Sports wenyewe watakuwa mwenyeji wa Toto Africans ya Mwanza katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga.

No comments:

Post a Comment