Pages

Friday, September 11, 2015

SIMBA SC KUMKOSA IBRAHIM HAJIB KESHO MKWAKWANI DHIDI YA AFRICAN SPORTS


SIMBA SC itamkosa mshambuliaji wake hatari, Ibrahim Hajib katika mchezo wake wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kesho dhidi ya African Sports Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Hajib, mkali wa mabao wa Msimbazi, pamoja na viungo Jonas Mkude na Abdi Banda wote ni majeruhi na hawajasafiti na timu Tanga kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kuwa mkali.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE jana, Nahodha wa timu hiyo, Mussa Hassan 'Mgosi' amesema kwamba wamefika salama Tanga na jana jioni walifanya mazoezi mepesi kwa ajili ya kuendelea kujiweka 'fiti' kuwavaa African Sports hapo kesho.
Ibrahim Hajib (kushoto) atakosekana Simba SC ikimenyana na African Sports kesho Mkwakwani

Mgosi alisema kwamba Simba imeimarika na iko tayari kusaka pointi tatu katika mchezo huo wa kwanza ili kujitengenezea mazingira ya ushindi kwenye mchezo unaofuata.
Mshambuliaji huyo aliyerejea Simba akitokea Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro msimu huu amesema kwamba mazoezi waliyofanya kujiandaa na ligi hiyo yalikuwa magumu na lengo lake ni kuhakikisha 'wanaiva' na kupata ushindi katika kila mechi watakayocheza.
Aliwataka wanachama na mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi kujitokeza kwa wingi
kuwashangilia kwa sababu huu ni mwaka mwingine na wamepanga kurejesha heshima ya timu.
"Tumeshafika Tanga, tuko vizuri, hatuna wasiwasi, mashabiki waje wasiogope, timu iko vizuri na wengine uwepo wetu ni muhimu, watu tuna nyota za ushindi," alisema Mgosi ambaye aliwahi pia kuchezea DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kwa hisani ya Bin Zubeiry

No comments:

Post a Comment