Pages

Wednesday, September 23, 2015

MIAKA 8 MFULULIZO, MECHI 15 MFULULIZO LIGI KUU SIMBA IMECHEZA BILA KUPOTEZA DHIDI YA YANGA

Simba vs Yanga

Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Bado tunaendelea kutazama rekodi mbalimbali zilizopita baina ya klabu za Simba na Yanga klabu hizi hasimu Tanzania zitavaana tena Jumamosi hii katika mchezo wa raundi ya nne wa ligi kuu bara. 
Kuelekea mchezo huo, Yanga haijapata ushindi dhidi ya Simba tangu Mei, 2013 waliposhinda 2-0. Hiyo inamaanisha kwamba mabingwa hao mara nyingi zaidi bara wataingia uwanjani kusaka ushindi wao wa kwanza ndani ya miaka miwili.
Je, unajua ya kwamba Simba imewahi kucheza gemu 15 mfululizo za ligi kuu dhidi ya Yanga pasipo kupoteza?. Kati ya Septemba 1, 2001 hadi April 27, 2008 Simba ilikuwa haijui suala la kupoteza mchezo wa Dar es Salaam Derby.
CHEKI MATOKEO YA GEMU 15 MFULULIZO AMBAZO SIMBA HAIKUPOTEZA DHIDI YA YANGA KATIKA LIGI KUU BARA PEKEE
Septemba 1, 2001, Simba 1-0 Yanga
Goli pekee la mshambulizi aliyekuwa na misuli na uwezo wa kupiga mashuti makali, Joseph Kaniki ’Golota’ katika dakika ya 76 lilisimama hadi mwisho. Yanga ilipoteza mchezo huo uliopigwa uwanja wa Uhuru. Ikumbukwe kabla ya timu hizo kuvaana mara mbili mwaka 2000. Simba walishinda 2-1 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza April 23.  Yanga wakashinda 2-0 katika gemu ya marejeano Agosti 5.
Septemba 30, 2001. Yanga 1-1
Joseph Kaniki alifunga goli lake la pili katika Dar es Salaam Derby dakika ya 65′. Zikiwa zimesalia dakika 4 gemu kumalizika, Sekilojo Chambua akaisawazishia Yanga na kutengeneza sare ya kufungana 1-1.
Agosti 18,2002, Simba 1-1 Yanga
Dakika ya 65′ iliendelea kuwa mbaya kwa Yanga kwani safari hii, Madaraka Suleimani ‘ Mzee wa Kiminyio’ alifunga goli la kuongoza upande wa Simba lakini kwa mara nyingine, Sekilojo Chambua akaisawazishia timu yake dakika moja kabla ya kumalizika kwa mchezo na kutengeneza matokeo ya 1-1.
Novemba 10, 2002, Yanga 0-0 Simba
Ilikuwa sare ya tatu mfululizo katika ligi kuu na mechi ya kwanza isiyo na magoli katika karne mpya.Septemba 28, 2003, Simba 2-2 Yanga.
 Ilikuwa moja ya mechi za kuvutia mwanzoni mwa miaka ya 2000. Simba ilikuwa mbele kwa magoli 2-0 kufikia dakika ya 36 kupitia kwa mshambulizi wake, Emmanuel Gabriel dakika za 27′ na 36′.
Kiungo mshambuliaji, Kudra Omari akapunguza presha kwa wapenzi wa timu yake baada ya kufunga zikiwa zimesalia dakika 3 mchezo kwenda mapumziko. Mshambulizi, Hernry Morris akaisawazisha Yanga dakika ya 55′ na hadi mwisho wa mchezo matokeo yalikuwa 2-2.
Novemba 2, 2003, Yanga 0-0 Simba.
Ilikuwa mechi mbaya licha ya Simba kuwa na msimu mzuri katika michuano ya kimataifa. Ilikuwa sare ya tano mfululizo huku ukiwa mchezo wa sita mfululizo Yanga wanashindwa kupata ushindi. Mechi ilimalizika kwa suluhu-tasa.
Agosti 7, 2004, Simba 2-1 Yanga
Mshambulizi raia wa DR Congo, Pitchou Kongo alifunga goli la kuongoza upande wa timu yake dakika ya 48′. Yanga iliongoza mchezo wa Dar es Salaam derby kwa mara ya kwanza tangu April 23, 2000 lakini wakajikuta wakipoteza tena mchezo. Idd Moshi alifunga dakika ya 4′ lakini, Steven Mapunda ‘ Garrincha’ akafunga mara mbili dakika za 59′ na 72′ na kuisaidia Simba kushinda 2-1 msimu wa mwaka 2000.
Baada ya Pitchou kufunga Simba walitulia na kufuga Simba wakapata magoli mawili ya ‘ chap chap’ kupitia kwa kiungo, Shaaban Kisiga dakika ya 64′ na Ulimboka Mwakingwe dakika ya 76′ na kushinda mechi.
Septemba 18, 2004, Yanga 0-1 Simba
Moja ya magoli maridadi ambayo yatakumbukwa sana katika mipambano ya Simba na Yanga ni lile lililofungwa na Athumani Machuppa dakika ya 84′ akiwa amepokea pasi na Suleimani Matola ambaye alikimbia haraka na mpira kutoka katika eneo lao la kujilinda, Matola ‘ alipunguza’ uwanja, Machuppa alikuwa amebaki mbele peke yake na walinzi, Samson Mwamanda na Salum Athuman (kama kumbukumbuka ziko sawa).
Kilichokuja kutokea ni goli kali. Alikimbilia pasi ya Matola na huku akikokota mpira kwa kasi akitoke wing ya kushoto, Machuppa alimpiga chenga ya hatari Mwamanda ambaye aliteleza na kubaki akimtazama Machuppa akipeleka mpira katika ‘angle’ na kuimaliza mechi. Baada ya mechi hiyo mahusiano ya Mwamanda na Yanga yakaingia doa na pengine alivuliwa thamani yake yote kiuchezaji .
 April 17, 2005, Simba 2-1 Yanga
Katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Simba ikiwa chini ya kocha wa muda, Jamhuri Kihwelo ‘ Julio’ sambamba na Boniface Pawassa katika benchi ilishinda 2-1. Yanga walitangulia kuongoza kupitia kwa kiungo Aaron Nyanda dakika ya 39′ lakini mshambulizi aliyekuwa na umbo kubwa, Nurdin Msiga akasawazisha dakika moja kabla ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza. Athumani Machuppa akazamisha goli la pili dakika ya 64′.
Agosti 21, 2005, Yanga 0-2
Simba. Ilikuwa gemu ya mwisho ya Dar es Salaam derby kwa nahodha-mshindi, Matola na kiungo mshambulizi, Nico Nyagawa akatupia kambani mara mbili katika dakika za 22′ na 56′ katika uwanja wa Sheikh Amir Abeid, Arusha na kuipa Simba ushindi wa 2-0. Baada ya mechi hiyo Matola aliruhusiwa kujiunga na Super Sport United ya Afrika Kusini.
Machi 26, 2006, Simba 0-0 Yanga
 Baada ya kupoteza mechi nne mfululizo Yanga walilazimisha suluhu-tasa katika gemu ya kwanza msimu wa 2006.
Oktoba 29, 2006, Yanga 0-0 Simba
Mechi hii ya marejeano ilimalizika kwa suluhu-tasa pia hivyo kutengeneza matokeo ya kutofunga katika michezo yo.
FAINALI LIGI KUU NDOGO, Jula 8, 2007, Simba 1 ( 5)-1 ( 4) Yanga
Shirikisho la mpira wa miguu nchini, TFF liliamua kurekebisha kalenda yake ya mashindano na hapo wakahitaji kuachana na mfumo wa zamani wa uendeshaji wa ligi kuu kutoka Machi-Septemba na kuwa, Agosti -Mei, ili kuendana na kalenda za kimataifa, hivyo ili kupata wawakilishi wa nchi katika michuano ya kimataifa timu za ligi kuu zikapangwa katika makundi, kisha hatua ya nusu fainali na fainali ikawakutanisha mahasimu Simba na Yanga katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Mshambulizi, Mkenya, Moses Odhiambo akaifungia Simba goli la kuongoza kwa mkwaju wa penalti dakika ya 2′ tu ya mchezo lakini, kiungo mshambulizi, Said Maulid ‘ SMG’ akaisawazisha Yanga dakika ya 55′ na mechi ikamuuliwa kwa mikwaju ya penalti na Simba wakashinda 5-4.
Oktoba 24, 2007, Simba 1-0 Yanga
Yanga walijikuta wakifungwa mechi ya tatu mfululizo na Simba katika gemu za Jamhuri Stadium, Morogoro. Safari hii walimalizwa na Ulimboka Mwakingwe dakika ya 32′ kwa kiki ya chini chini  iliyompita goliki, Ivo Mapunda katika ‘ kwapa zake’. Baada ya kipigo hicho Ivo a aliyekuwa mlinzi wa kulia Shadrack Nsajigwa wakasimamishwa miezi 6 na klabu yao.
April 27, 2008, Yanga 0-0 Simba
Simba ilifikisha gemu ya 15 mfululizo pasipo kupoteza mbele ya mahasimu wao kwa kulamisha suluhu-tasa. Hadi kufikia gemu hii, Simba ilikuwa imeshinda mara 7 mechi nyingine zilimalizika kwa sare.

No comments:

Post a Comment