Pages

Tuesday, September 15, 2015

MGOSI ASEMA WACHEZAJI SIMBA SC WAPO TAYARI KIMWILI NA KIAKILI KWA AJILI YA MGAMBO KESHO MKWAKWANI

Nahodha wa Simba SC, Mussa Hassan Mgosi amesema wachezaji wako tayari kimwili na kiakili kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Mgambo Mkwakwani

Na Princess Asia, TANGA
NAHODHA wa Simba SC, Mussa Hassan Mgosi amesema kwamba wachezaji wako tayari kimwili na kiakili kwa ajili ya mchezo wa kesho dhidi ya wenyeji Mgambo JKT Shooting.
Simba SC iliyoweka kambi katika hoteli ya Mtendele hapa Tanga, kesho inaingia katika mchezo wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mgambo, baada ya awali kushinda 1-0 dhidi ya African Sports ya hapa pia.
Na Nahodha wa Wekundu hao wa Msimbazi, Mgosi amesema kwamba anafurahi baada ya mazoezi ya leo asubuhi wachezaji wote ukitoa beki Samih Hajji Nuhu wako vizuri.
“Timu iko vizuri na wachezaji wote tuko vizuri kimwili na kiakili kuelekea mchezo wa kesho. Tunafahamu mchezo utakuwa mgumu kwa sababu ya historia yetu na Mgambo na pia mechi za Tanga kwa ujumla, lakini tumejipanga,” amesema Mgosi.
Mshambuliaji huyo aliyewahi kuchezea pia DC Motema Pembe ya DRC, amesema kwamba wamedhamiria kushinda mechi zao zote awali hapa Tanga ili kujijengea hali ya kujiamiani katika mbio za ubingwa.
Amesema kwamba baada ya takriban wiki moja ya kuwa Tanga wachezaji wote wamezoea hali ya mkoa huu na hawana wasiwasi wowote kuelekea mchezo wa kesho.
Mgosi amefurahia kupona kwa beki Hassan Isihaka na mshambuliaji Ibrahim Hajib akiamini kutampa wigo mpana kocha Dylan Kerr kuchagua wachezaji wa kuanzisha kesho Mkwakwani.
“Nafurahi wachezaji wenzetu ambao walikuwa majeruhi wakati tunakuja huku, Hassan na Hajib wote wako fiti na tumefanya nao mazoezi jana na leo vizuri na hii itampa fursa nzuri kocha kuchagua wachezaji wa kutumia,”amesema.
Mbali na Simba SC na Mgambo, kutakuwa na mechi nyingine sita za Ligi Kuu kesho; Uwanja wa Kambarage, Shinyanga wenyeji Stand United wataikaribisha Azam FC na mabingwa watetezi Yanga SC wataikaribisha Prisons ya Mbeya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho.
Kagera Sugar walioanza kwa ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya Mbeya City, watasogea kilomita kadhaa mbele Nyanda za Juu Kusini hadi Ruvuma kwenda kumenyana na Majimaji FC mjini Songea ambayo nayo ilianza na ushindi wa 1-0 dhidi ya JKT Ruvu.
Mechi nyingine za Ligi Kuu kesho ni kati ya Mbeya City na JKT Ruvu Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Toto Africans na Mtibwa Sugar Uwanja CCM Kirumba mjini Mwanza na Ndanda FC dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara. 
Mechi za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara zitakamilishwa keshokutwa kwa mchezo kati ya Mwadui FC dhidi ya African Sports Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Kwa hisani ya Bin Zubeiry blog

No comments:

Post a Comment