ARSENAL BADO INAHITAJI KUSAJILI WACHEZAJI WAWILI
ARSENAL inahitaji kusajili wachezaji wawili zaidi kuwa
katika nafasi nzuri ya kushindania ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu huu.
Kwa
msingi huo naenda tofauti kidogo na maoni ya nguli wa zamani wa klabu hiyo
anayesema mara kwa mara kuwa wanahitaji kusajili kila idara ili kuweza
kushindana na Chelsea, Manchester City na Manchester United kwenye
kinyang’anyiro cha ubingwa.
Tayari
Profesa Arsene Wenger ameimarisha eneo moja la golikipa kwa kumsajili Petr Cech
kutoka Chelsea na kipa huyo alionesha uwezo mkubwa kwenye mechi ya Ngao ya
Hisani dhidi ya timu yake ya zamani ambapo Arsenal ilishinda kwa bao 1-0.
Cech
alionesha utulivu langoni, alikuwa kama kiongozi na zaidi aliwanyima Chelsea
mabao ya wazi kutokana na umahiri wake kiasi cha kuthibitisha kuwa kweli
Arsenal ilihitaji mtu wa aina yake katika eneo hilo.
Kwa
mtazamo wangu Arsenal bado inahitaji kusajili mfumania nyavu mahiri na zaidi
kiungo mkabaji atakayesaidiana na Francis Coquelin ambaye kama Petr Cech naye
alikuwa imara katika eneo la kiungo kiasi cha kuwapoteza Nemanja Matic, Ramires na Francesc Fabregas.
Ushindi
wa mabao 2-0 kwenye Ligi Kuu dhidi ya Manchester City, ushindi wa mabao 2-1
dhidi ya Manchester United kwenye Kombe
la Chama cha Soka cha England (FA) na sasa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Chelsea
kwenye Ngao ya Hisani ni uthibitisho tosha kuwa Arsenal wako tayari kabisa kwa
mbio za ubingwa msimu ujao.
Moja
ya shida kubwa ya Arsenal miaka kadhaa iliyopita ilikuwa ni kupata ushindi
kwenye mechi kubwa kama dhidi ya Manchester United, Manchester City na Chelsea,
shida hiyo sasa inaonekana kuondoka na kuelekea zama mpya.
Wenger
anafahamika kuwa bado yuko sokoni akiwinda saini ya mfumania nyavu mahiri
atakayepatikana hasa Karim Benzema kutoka Real Madrid, lakini binafsi
namuongeza na Wiliam Calvarhlo kutoka Sporting Lisbon ya Ureno.
Arsenal
inahitaji watu hawa wawili ili wasiendelee tena kusubiri zaidi mafanikio hasa
ya kunyakua taji la Ligi Kuu ya England
ambalo ndio hasa kiini cha Arsene Wenger kushambuliwa mara kwa mara na Jose
Mourinho.
Haihitaji
zaidi ya maeneo hayo kwani tayari ina timu iliyokaa pamoja kwa muda mrefu na
muunganiko wa kitimu ndio kitu cha msingi zaidi kuliko kununua lundo la
wachezaji na kuwauza baada ya msimu mmoja.
Hakuna
msimu ambao Aaron Ramsey ama Jack Wilshere hawawi majeruhi na ndio msingi wa
Wenger kutakiwa kuleta kiungo mkabaji atakayeweza kucheza kama nyota hao wawili
watakapokuwa majeruhi. Lakini kwa eneo la ushambuliaji bado inahitaji mtu
atakayeweza kufunga mabao 20 kwa msimu.
Akipatikana
mshambuliaji wa aina hiyo ataweza kusaidiana na akina Alexis Sanchez na Olivier
Giroud na kuhitimisha ukame wa kushinda taji la Ligi Kuu ya England ambalo mara
ya mwisho ni msimu wa mwaka 2002/2003. Kinyume chake bado ataendelea kusubiri
na kutoa mwanya kwa hasimu wake mkubwa Jose Mourinho kumshambulia.
No comments:
Post a Comment