Pages

Saturday, July 11, 2015

Yanga imekamilika kwa michuano ya Kombe la Kagame

Kikosi cha Yanga Africans.
Na Mwandishi Wetu
KOCHA mkuu wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga, Hans van der Pluijm amesema kuwa, licha ya kupata ushindi mdogo wa 1-0 dhidi ya KMKM ya Zanzibar juzi kwenye Uwanja wa Taifa, lakini kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame.
Pluijm alisema licha ya upungufu mdogo uliojitokeza, ana matarajio makubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo na hata kulibakiza kwenye ardhi ya Tanzania kombe hilo ambalo linawaniwa na timu 13.
Michuano ya Kombe la Kagame inatarajia kuanza jijini Dar es Salaam Julai 18 kwenye Uwanja wa Taifa.
Akizungumza juzi Pluijm alisema kikubwa kilichomvutia katika mechi tatu za kirafiki walizocheza ni namna ambavyo timu hiyo ilivyokuwa na uwiano baada ya kuziba nafasi za wachezaji ambao wameachana nao baada ya msimu uliopita kumalizika.
Naweza kusema hiki ndicho kikosi changu bora ukilinganisha na kile kilichobeba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kila mchezaji tuliyekuwa naye msimu huu ana kitu cha ziada na wamekuwa na ushirikiano mzuri pamoja na wale wageni, alisema Pluijm.
Mholanzi huyo pia alisema amefurahishwa na kiwango kilichooneshwa na mshambuliaji mpya raia wa Zimbabwe, Donald Ngoma ambaye ndiye aliyefunga bao hilo pekee katika mchezo na KMKM na kusema atakuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi chao na ni mmoja ya washambuliaji anayemtegemea kufunga mabao mengi msimu huu.

No comments:

Post a Comment