Pages

Tuesday, June 9, 2015

TFF YAMALIZA UTATA WA MKATABA BAINA YA MESSI NA SIMBA




Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Selestine Mwesigwa (kulia) akiongea na waandishi wa habari juu ya kumalizika kwa sakata la utata wa mkataba wa Ramadhan Singano na klabu ya Simba leo. Katikati ni mchezaji Ramadhan Singano na kushoto ni Mkurugenzi wa Uanachama wa TFF, Eliud Mvera. (Picha na Rahel Pallangyo)

Ramadhan Singano akiongea na wandishi leo

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetumia busara kumaliza sakata la mkataba wa mchezaji wa Simba Ramadhan Singano na uongozi wa Simba
Akizungumza na wandishi wa habari Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa alisema kuwa TFF imekutana na Simba na Ramadhani Singano na kumaliza utata uliokuwepo kwenye mkataba wa mchezaji huo bila kusema ni utata upi kwani swala la mkataba ni la mchezaji na klabu yake.
Alianza kwa kusema kumekuwa na maneno mengi , kumekuwa na vichwa vya habari vingi na simu kuhusu swala la mahusiano ya mkataba wa Ramadhan Singano na Simba na TFF ikaingilia kati swala hilo ambapo kwenye kikao hicho Simba iliwakilishwa na mjumbe wa kamati ya Utendaji Collin Frich na Singano alikuwa ameambatana na Mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji  (SPUTANZA)
 “TFF imeamua utata uliokuwepo kwenye mkataba kati yao na mchezaji Ramadhan Singano umalizwe kwa kuingia mkataba na pande zote mbili zimeridhia”, alisema Mwesigwa bila kueleza kwa kina bali alisisitiza kuwa mkataba wa ajira ni kati ya mwajiriwa na mwajiri
Pia Mwesigwa alisema kuwa TFF ina mkataba mama ambao vilabu na wachazeji wanatakiwa kuufuata kama mfano wakati wa kuingia mkataba na klabu na kuwataka wachezaji kuelewa mkataba kabla ya kutia saini.
Mwesigwa alisema kuwa wamewaita Simba na Singano ili kutapata suluhu na siyo kupata mshindi  bali kuhakikisha mchezaji na klabu kila mmoja anapata masilahi yake kwani tofauti ilikuwa kwenye mkataba kulingana na mkataba mama.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha wachezaji (SPUTANZA), Mussa Kisoki alisema  amefurahi kupatikana suluhu kati ya mchezaji Ramadhan Singano na Simba na kupongeza TFF kwa kuingilia kati.
“Nimeridhika kwa matokeo ya mazungumzo ya pande zote mbili kwani tofauti ndogo tu imegundulika na Messi ni mchezaji halali wa Simba hadi hapo watakapoingia mkataba”, alisema
Pia alisema kuwa hakuna mahali ambapo mkataba ulikuwa umeghushiwa bali tofauti ilikuwa ndogo sana na amefurahi kwa upatanishi uliopatikana kwani
Naye msemaji  wa Simba Hajji Manara alisema yeye hana cha kuongeza kwenye maamuzi yao na kuwasisitiza wandishi kuheshimu maamuzi ya TFF
“TFF ndio wenye mpira wao na wamefanya maamuzi ambayo tunatakiwa kuyaheshimu”, alisema Manara huku akiingia kwenye gari .
Kwa upande wake mchezaji Ramadhan Singano alisema kuwa anamwachia Mungu huku akisisitiza kuwa yeye ni mchezaji huru huku uso wake ukionyesha kutoridhika na maamuzi.
“Mimi sina zaidi bali namwachia Mungu lakini natambua mimi ni mchezaji huru kwani mkataba niliokuwa nao unamalizika Julai”, alisema Singano maarufu kama Messi.
Takribani  mwezi mmoja sasa Ramadhan Singano amekuwa akilalamikia utata wa mkataba uliokuwapo kwenye mkataba wake na klabu yake ya Simba ambapo yeye alikuwa akidai mkataba wake unamalizika Julai mwaka huu huku klabu yake ikisema mkataba wake na mchezaji huyo unamalizika Julai 2016.


No comments:

Post a Comment