Pages

Friday, January 16, 2015

MCHEZAJI WA ZAMANI WA YANGA JOHN MWANSASU ATEULIWA KUWA KOCHA WA TIMU YA TAIFA



SHIRIKISHO la Soka Tanzania(TFF) limemteua mchezaji wa zamani wa Yanga John Mwansansu kuwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Soka la Ufukweni, akisaidiana na Ally Sharif wa Zanzibar.
Akitangaza uteuzi huo jana Mwenyekiti wa Kamati ya Soka la Ufukweni wa TFF Ahmed  Mgoi alisema Mwansansu  na msaidizi wake huyo watakuwa na kazi ya kuchagua wachezaji wa timu ya taifa wa soka la ufukweni ambao watajiandaa na michuano ya Afrika.
Kwa mujibu wa Mgoi, fainali za michuano ya  Afrika ya mchezo huo yatarajiwa kufanyika April Mwaka huu Sheli sheli.
Alisema ili Tanzania iweze kufunzu imepangwa kucheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Kenya utakaochezwa nchini humo kati ya  Februari 13 na 15 kisha kucheza mchezo wa marudiano Dar es Salaam kati ya Februari 20, 21 na 22.
“Tanzania  tutashiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza, hivyo baada ya kumpata Kocha tutaanza maandalizi ya kusaka nafasi hiyo, tushiriki kwenye fainali za Afrika,”alisema.
Mgoi alisema kikosi cha timu ya Taifa kitaundwa na wachezaji waliofanya vizuri kwenye mashindano ya vyuo vikuu yaliyofanyika Zanzibar mwaka jana, ambapo watatajwa hivi karibuni kisha kuingia kambini.
Alisema wachezaji wa Zanzibar na Tanzania Bara wataungana katika kambi ya pamoja na kucheza michezo ya kirafiki ambapo baadaye watachaguliwa wachezaji watakounda timu ya taifa kwa ajili ya michuano hiyo.
“Kikosi kitatangazwa na Mwansansu kuanzia Januari 19, mwaka huu, kwa upande  wa Zanzibar tayari wanajulikana kwa vile walianza muda mrefu na mazoezi ya pamoja na timu ya Zanzibar yatafanyika Januari 24 na 25 mwaka huu,”alisema.

Alisema iwapo watafanikiwa kuitoa Kenya kwenye hatua za awali, watakutana na Misri ambapo wakifanya vizuri, watakuwa wamefuzu kushiriki fainali za michuano hiyo.
Kuhusu viwanja vitakavyotumika, alisema atataja viwanja vinne baadaye ambapo watawekeza, kwani ndio kwanza wanaandaa mkakati wa maendeleo kwa ajili ya mchezo huo huku wakiendelea na mashindano.

No comments:

Post a Comment