Pages

Friday, January 9, 2015

KILUVYA UTD, NJOMBE BADO ZAKIMBIZA SDL

Kiluvya United ya Pwani na Njombe Mji ya mkoani Njombe ndizo timu pekee zilizomaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Daraja la Pili (SDL) kwa kushinda mechi zote katika makundi yao, hivyo kujipatia pointi 15 kila moja.

Njombe Mji imeongoza kundi D lenye timu za Mkamba Rangers ya Morogoro iliyofikisha pointi nane, Wenda ya Mbeya pointi sita, Volcano FC ya Morogoro pointi sita, Town Small Boys ya Ruvuma pointi tano na Magereza ya Iringa yenye pointi moja.

Katika kundi C, Kiluvya United inafuatiwa na Mshikamano ya Dar es Salaam yenye pointi kumi, Abajalo pia ya Dar es Salaam pointi saba, Cosmopolitan na Transit Camp za Dar es Salaam ambazo kila moja imemaliza mzunguko huo ikiwa na pointi tano. Kariakoo ya Lindi haina pointi.

Mji Mkuu (CDA) ya Dodoma na Singida United ya Singida ndizo zinazochuana katika kundi A kila moja ikiwa na pointi nane. Mvuvuma FC ya Kigoma yenye pointi tano ndiyo inayofuatia, wakati Milambo ya Tabora ina pointi nne huku Ujenzi Rukwa ikikamata mkia kwa pointi moja.

Pia mchuano mkali uko katika kundi B ambapo JKT Rwamkoma ya Mara na Mbao FC ya Mwanza ziko kileleni kila moja ikiwa na pointi tisa. AFC ya Arusha inafuatia kwa pointi sita, Bulyanhulu FC ya Shinyanga ina pointi nne wakati Pamba FC ya Mwanza iko mkiani kwa pointi moja.

Mzunguko wa pili wa ligi hiyo itakayotoa timu nne zitakazopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao (2015/2016) utaanza kutimua vumbi Januari 24 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment