Pages

Friday, August 29, 2014

KOZI YA UKUFUNZI WA UTAWALA YA FIFA KUFANYIKA DESEMBA NA MTIHANI WA WAAMUZI, MAKAMISHNA SEPTEMBA 5

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) wameandaa kozi ya ukufunzi wa utawala itakayofanyika Desemba mwaka huu.
Kozi hiyo itakayoendeshwa na wakufunzi kutoka FIFA itafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Desemba 1 hadi 5 mwaka huu, ambapo sifa ya chini ya elimu kwa wanaotaka kushiriki ni kidato cha nne.
Kwa wanaotaka kushiriki kozi hiyo wanatakiwa kutuma maombi yao kwa Katibu Mkuu wa TFF. Mwisho wa kupokea maombi hayo ni Septemba 5 mwaka huu ambapo wanatakiwa pia kuwasilisha nakala za vyeti vyao vya kitaaluma.
MTIHANI WA WAAMUZI, MAKAMISHNA SEPTEMBA 5
Mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test) kwa waamuzi wanaotaka kuchezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu huu utafanyika katika vituo viwili kuanzia Septemba 5-6 mwaka huu.
Waamuzi watakaoshiriki mtihani huo ni wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na wale wa class one. Pia kutakuwa na semina wa makamishna wanaotaka kusimamia mechi za VPL na FDL ambayo itafanyika Septemba 7 mwaka huu.
Vituo vya mtihani huo ni Dar es Salaam na Shinyanga. Kituo cha Dar es Salaam ni kwa waamuzi na makamishna kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kilimanjaro, Lindi, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Njombe, Pwani, Ruvuma na Tanga.
Kituo cha Shinyanga ni kwa waamuzi na makamishna kutoka mikoa ya Arusha, Geita, Kagera, Katavi, Kigoma, Manyara, Mara, Mwanza, Rukwa, Shinyanga, Simiyu, Singida na Tabora.
Waamuzi wote ambao wamechezesha VPL na FDL msimu wa 2013/2014 na kupata matatizo au kuondolewa kwenye ligi hawahusiki na mtihani huo. Washiriki wanatakiwa kufika kituoni siku moja kabla.
Wasimamizi ni Charles Ndagala, Israel Mujuni, Issarow Chacha, Joan Minja, Pascal Chiganga, Riziki Majala, Said Nassoro, Salum Chama, Soud Abdi, Victor Mwandike na Zahara Mohamed.

No comments:

Post a Comment