Pages

Saturday, July 5, 2014

Mafunzo ya matumizi ya tiketi za elektroniki kwa wadau wa mpira wa miguu mkoani Mbeya yafanyika.


 Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeendesha mafunzo ya matumizi ya tiketi za elektroniki kwa wadau wa mpira wa miguu mkoani Mbeya.
Mafunzo hayo yamefanyika jana na leo (Julai 4 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Sokoine, na kushirikisha wasimamizi wa mechi, viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA) na makatibu na maofisa habari wa klabu za Tanzania Prisons na Mbeya City.
Wengine walioshiriki mafunzo hayo ni Meneja wa Uwanja wa Sokoine na msaidizi wake, wasimamizi wa milangoni (Stewards) na waandishi wa habari wa mkoani Mbeya.
Mafunzo hayo yanahitimishwa kesho (Julai 5 mwaka huu) kwa mechi kati ya Tanzania Prisons na Mbeya City itakayochezwa Uwanja wa Sokoine kuanzia saa 10 kamili jioni. Kiingilio ni sh. 3,000, na tiketi zilianza kuuzwa Julai Mosi mwaka huu kupitia M-Pesa, CRDB Simbanking na maduka ya Fahari Huduma.
 TIMU za Tanzania Prison na Mbeya City zote za jijini Mbeya zimejipanga vizruri kwa ajili ya mchezo huo wa majaribio ya tiketi hizo.
 
Ndani ya Semina hiyo elekezi iliyotolewa kwa Waandishi wa habari Mkoa wa Mbeya na viongozi wa mpira wa miguu mengi yamezungumzwa ambapo changamoto kadhaa zilizo jitokeza hapo kabla sasa zimefanyiwa kazi na kuelezwa kuwa sasa ni wakati wa kujaribu tena kujua kama majibu yake yamepatikana.
Akizungumza katika Semina hiyo Mwezeshaji ambaye ni mtaalamu wa mitambo hiyo kutoka benki ya CRDB, Kurrington Chahe, alisema tiketi za mchezo huo zilianza kuuzwa siku tano kabla na ndivyo itakavyokuwa katika michezo yote ya ligi kuu.
Alisema lengo ni kumfanya shabiki kununua tiketi popote alipo hapa nchini kutokana na mfumo huo kufanyika kwa nia ya mtandao ambapo shabiki anaweza akanunua kwa njia ya mitandao ya simu ama kufika katika tawi la Benki ya CRDB.
Aliongeza kuwa lengo la kufunga mashine hizo ni kudhibiti mapato ya uwanjani ambapo fedha zote zitakuwa zikipitia moja kwa moja benki na kwa mawakala na sio mikononi mwa watu kama ilivyokuwa awali.
Alisema kutumika kwa mfumo huo pia kutaondoa wanaojiita stafu ili wapite bure pamoja na makomandoo wa timu wanaokaa milangoni na kuingiza watu bure.
Kwa upande wake Afisa Habari wa TFF, Bonifasi Wambura alisema mfumo huo ni mpya na unaweza ukawa na changamoto nyingi ndiyo maana wameandaa mechi ya kirafiki baina ya Mbeya city na Tanzania Prison ili kujaribu matumizi ya mitambo hiyo.
Alisema kiingilio katika mechi hiyo kitakuwa shilingi 3000 ambapo shabiki atafika na tiketi yake getini ambayo itaskaniwa kwenye mashine ili kubaini idadi ya watu wakaoingia uwanjani pamoja na mapato yake ambapo alisema utaratibu huo utaondoa usumbufu wa kuanza kuhesabu mapato baada ya mechi.
Wambura alisema tiketi zitasitishwa kuuzwa katika kipindi cha pili cha mchezo kinapoanza ili kuweza kurahisisha utaratibu mwingine kufanyika ambapo aliongeza kuwa mfumo huo utapunguza gharama nyingi zikiwemo magari ya kuuzia tiketi.
Katika mchezo huo Mawakala zaidi ya 15 wamefundishwa na kuteuliwa kuuza tiketi hizo kutoka Wilaya za Mkoa wa Mbeya na jijini hapa.

No comments:

Post a Comment