Pages

Saturday, March 1, 2014

YANGA YAVUNJA MWIKO KWA MWARABU, YAIFUNGA BAO 1-0 TAIFA







MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara Yanga wameweka historia mpya katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada kuifunga Al Ahly ya Misri kwa bao 1-0 kwenye mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo Yanga itahitaji ushindi ama sare ya aina yoyote pindi timu hizo zitakaporudiana katika kipindi cha wiki moja ijayo Cairo, Misri ili isonge mbele kwa hatua inayofuata ya mashindano hayo.
Yanga iliingia katika raundi ya pili ya mashindano hayo baada ya kuifunga Comorozine ya visiwa vya Comoro kwa mabao 7-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kisha kuibuka na ushindi wa mabao 5-2 kwenye mchezo wa marudiano.
Shujaa wa Yanga kwenye mechi ya jana alikuwa nahodha wa timu hiyo Nadir Haroub’Cannavaro’ aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na kiungo wa kimataifa wa Rwanda Haruna Niyonzima kwenye dakika ya 81 na kuamsha nderemo na vifijo kwa mashabiki wa timu waliofurika uwanjani kwenye mechi hiyo.
Ni miaka 29 imepita tokea timu ya Tanzania kuwafunga mabingwa hao mara nane wa Afrika kwani mara ya mwisho Simba iliifunga timu hiyo kwa mabao 2-1 kwenye mchezo mkali uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mwaka 1985 kwa mabao ya Zamoyoni Mogella na Mtemi Ramadhani.
Cannavaro ameingia kwenye historia ya nguli hao wa zamani wa kimataifa wa Tanzania kwa kuweza kufunga bao dhidi ya timu hiyo ambayo wiki iliyopita ilitoka kutwaa taji la Super Cup kwa kuifunga Csafien ya Tunisia kwa mabao 3-2.
Yanga ilianza mchezo huo kwa kasi na ilionekana kama wangeweza kupata mabao ya mapema lakini lakini kipa wa timu hiyo Sherif Ekramy Ahmed aliyokoa mpira wa kichwa uliopigwa na Emmanuel Okwi kwenye dakika ya 5 na kuwa kona butu.
Al Ahly walionekana kucheza taratibu na kufanya mashambulizi ya kushtukiza hali iliyofanya Yanga kutawala mchezo huo kwa kiwango kikubwa na katika dakika ya 20 nusura Hamisi Kiiza aifungie timu yake bao lakini alichelewa mpira wa krosi wa Simon Msuva toka wingi ya kulia.
Mohamedi Ismail alikosa nafasi nzuri kwenye dakika ya 28 baada ya kupokea mpira mzuri uliotokana na shambulizi la kushtukiza kutoka kwa kiungo wa timu hiyo Hossam Mohamedi akiwa amebanwa na beki Kelvi Yondani alipiga shuti lilitoka pembeni kidogo ya lango.
Kipindi cha pili Al Ahly walionekana kuchangamka kidogo hali iliyofanya kutawala mchezo huo hali iliyomlazimu kocha wa Yanga Hans Pluijm kumtoa Hamisi Kiiza na kumuingiza Didier Kavumbagu aliyeir ejesha Yanga mchezoni.
Huku kocha wa Ahly Ahly alimtoa kiungo Moussa Yedan na kumuingiza Mahmoud Ibrahim hata hivyo ni Yanga walionyesha dhamira ya kuibuka na ushindi kwenye mechi hiyo huku Al Ahly wakionekana kucheza kwa zaidii kwa kutafuta sare.
Okwi  kwenye dakika ya 70 alipokea pasi nzuri kutoka kwa Frank Domayo toka katikati ya uwanja aliwazunguka mabeki wa Al Ahly na kupiga shuti kali lililopanguliwa kipa wa Al Ahly Sherif Ekramy Ahmed  na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Kwenye dakika ya 81 Nadir Haroub’Cannavaro’aliunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliochongwa na Haruna Niyonzima na kuiandikia Yanga bao hilo muhimu kwenye mechi hiyo.
Kocha wa Yanga alimpumzisha winga Mrisho Ngassa na kumuingiza Saidi  Bahanunzi huku kocha wa Al Ahly alimpumzisha Mohamedi Ismail na kumuingiza Ahmedi Shakri mabadiliko ambayo hayakubadili sura ya mchezo huo.
Yanga Deogratius Munishi,Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub’Cannavaro’, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Simon Msuva, Haruna Niyonzima , Emmanuel Okwi, Mrisho Ngassa, Hamisi Kiiza.
Al Ahly: Sherif Ekramy Ahmed, Saadeldin Saad, Mohamedi Al Ghareeb, Ahmed El Moneima. Sayed Abdel Wahed, Shihab Eldin Saad, Ramy Abdel Aziz, Moussa Yedan, Mohamedi Ismail, Amri Gamal Sayed.

No comments:

Post a Comment