Pages

Wednesday, December 18, 2013

SIMBA YAPANGWA KUNDI MOJA NA AFC LEOPARDS YA KENYA NA KCC UGANDA KOMBE LA MAPINDUZI



KAMATI ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi, imetangaza makundi na ratiba ya hatua ya awali ya michuano hiyo inayofanyika kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar Januari mwakani.

Hata hivyo, ratiba hiyo haioneshi uwepo wa timu kutoka nchi za Vietnam, China na Oman ambazo awali ilitangazwa kuwa zimealikwa kushiriki patashika hizo.
Ratiba iliyotolewa na kamati hiyo, inaonesha kuwa jumla ya timu 12 zitaumana kuwania taji hilo, ambazo zimegawiwa katika makundi matatu, kila moja ikiwa na timu nne.

Timu hizo ni Mbeya City, Pemba Combine, Chuoni na URA kutoka Uganda ambazo zinaunda kundi A, huku kundi B likiwa na timu za Simba, KMKM, AFC Leopards ya Kenya pamoja na KCC kutoka Uganda.

Mabingwa watetezi wa michuano hiyo Azam FC watakuwa katika kundi C pamoja na makamu bingwa Tusker ya Kenya, Yanga SC na Unguja Combine.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, pazia la ngarambe hizo litafunguliwa Januari 1, 2014, kwa mechi mbili za kundi B katika uwanja wa Amaan, ambapo wakati wa saa 10:00 mabaharia wa KMKM watapambana na Manispaa ya jiji la Kampala (KCC).
Aidha saa 2:00 usiku, wekundu wa Msimbazi Simba SC, watakuwa kibaruani dhidi ya AFC Leopards.

Januari 2, 2014, kutakuwa na mechi nne, katika kila uwanja, kati ya Amaan Unguja na  Gombani Pemba, kutakuwa na michezo miwili.
Zile za Amaan, ni kati ya Azam FC na Unguja Combine (saa 10:00 jioni) na Yanga dhidi ya Tusker itakayorindima kuanzia saa 2:00 usiku, na huko Gombani shughuli itakuwa kati ya URA na Chuoni (kundi C) watakaovaana saa 8:00 mchana, huku Mbeya City ikitoana jasho na Pemba Combine, saa 10:00 jioni katika mchezo wa kundi A.

Fainali ya ngarambe hizo itapigwa uwanja Amaan Januari 12 wakati wa saa 2:00 usiku, ambayo ndiyo kilele cha maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment