Pages

Thursday, December 19, 2013

OKWI AMALIZA MZIZI WA FITINA, ATUA DAR TAYARI KUANZA KAZI YANGA

HATIMAYE mshambuliaji Emmanuel Arnold Okwi amewasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam jioni hii tayari kuanza kuutumikia Mkataba wake wa miaka miwili ndani ya klabu ya Yanga SC ya Tanzania. 
Okwi alitua kwa ndege ya RwandaAir Saa 9:55 jioni na kulakiwa na viongozi na wapenzi kadhaa wa timu hiyo JNIA kabla ya kupakiwa kwenye gari ndogo aina ya saluni alilokuwa akiendesha Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa ya Yanga, Seif Ahmed ‘Magari’ na kuondoka. Alikaa kiti cha nyuma na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Mussa Katabaro. 
Okwi katikati baada ya kuwasili JNIA akiwa na Katabaro kulia na Bin Kleb kushoto jioni hii na chini akionyesha jezi namba 25

Okwi alitokea geti la wageni maalum la JNIA na kusindikizwa na Polisi huku, umati wa mashabiki wa Yanga ukimshangilia na kumfanya atoke kwa taabu hadi kupanda gari. 
Mara tu baada ya kutoka nje ya JNIA, Okwi alisema; “Nimekuja Yanga kufanya kazi,” na alipoulizwa kuhusu utata wa usajili wake, akasema; “Mimi nimekuja kufanya kazi, hayo mengine, mamlaka husika zitajua,”alisema Okwi aliyekuwa amevalia jezi nambari 25 ya Yanga.   
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdaollah Ahmed Bin Kleb alisema kwamba mchezaji huyo anakwenda moja kwa moja kambini, Protea Hotel kuungana na wenzake tayari kwa mchezo wa Jumamosi wa Nani Mtani Jembe dhidi ya mahasimu, Simba SC. 
Simba na Yanga zitamenyana Jumamosi katika mchezo ambao iwapo dakika 90 zitamalizika kwa sare, mikwaju ya penalti itaamua mshindi.
Mchezo huo, unaoandaliwa na wadhamini wa klabu hizo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager, unatarajiwa kuchezeshwa na refa Ramadhan Ibada ‘Kibo’ kutoka Zanzibar, atakayesaidiwa na Ferdinand Chacha wa Bukoba na Simon Charles kutoka Dodoma, wakati refa wa akiba atakuwa Israel Nkongo wa Dar es Salaam na mtathimini wa waamuzi ni Soud Abdi wa Arusha.
Okwi akizungumza na Waandishi wa Habari
Anatoka kuelekea kwenye gari
Anasindikizwa na Polisi
Ndani ya gari kiti cha nyuma na Katabaro
Dereva Seif Magari anaondoa gari 'mdogo mdogo'

Jumapili Yanga SC ya Dar es Salaam ilitangaza kumsajili Okwi raia wa Uganda kwa Mkataba wa miaka miwili na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya klabu hiyo, Abdallah Ahmed Bin Kleb alisema Okwi ataanza kuichezea timu hiyo mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara na michuano ya Afrika.
Etoile du Sahel ya Tunisia ilimnunua Okwi kutoka Simba SC Januari mwaka huu kwa dola za Kimarekani 300,000, lakini mchezaji huyo akaamua kuachana na klabu hiyo na kurejea kupumzika kwao Uganda, kwa madai hakulipwa mishahara kwa miezi mitatu.
Wakati huo huo, Etoile hadi sasa haijailipa Simba SC fedha zake za kumnunua mchezaji huyo na sakata lake limefikishwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Baada ya Okwi kukaa bila kucheza kwa miezi sita, Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA) lilimpigania aruhusiwe kurejea nyumbani kuichezea SC Villa ya huko ili kunusuru kiwango chake. 
Hata hivyo, baada ya kung’ara na timu ya taifa ya Uganda ‘The Ceanes’ nchini Kenya kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge mwezi huu, Okwi amesajiliwa Yanga SC.
Bin Kleb alisema kwamba walimsajili Okwi tarkiban siku sita zilizopita, lakini Hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ilipatikana Jumapili na ndiyo maana wakaamua kumtangaza.
Alipoulizwa kuhusu utata wa sakata lake ambalo limefika hadi FIFA, Kleb alisema; “Tumefuatilia kote, hadi kwa wanasheria, na tumefanikiwa kupata hadi ITC yake, nawaambia mashabiki wa Yanga wajue viongozi wao wanafanya kazi, hatuna stori nyingi, sisi tunafanya vitendo, tunafanya kazi kwa siri sana,”.
“Na tumepitia sehemu zote, tumeona kabisa tuko sahihi katika kumsajili mchezaji huyu na hakutakuwa na tatizo lolote upande wetu,”alisema. 
Lakini Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba watani wao wa jadi, Yanga SC wameingia mkenge kumsajili Okwi na labda watamtumia kwenye mchezo wa Nani Mtani Jembe pekee, lakini zaidi ya hapo hatacheza Jangwani kwenye michuano yoyote rasmi.
Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), alisema kwamba Okwi ni mchezaji halali wa Etoile du Sahel ya Tunisia na hawezi kucheza Yanga.
“Mimi sina wasiwasi, naangalia tu sarakasi zao nikiwa najua wataangukia wapi. Yule mchezaji Yanga wameingizwa mkenge na FUFA (Shirikisho la Soka Uganda). Kwa sababu, Etoile ilimtoa kwa mkopo SC Villa na ndiyo maana hata FUFA walipotaka kumtumia katika CHAN, wakaambiwa haiwezekani kwa kuwa yule ni mchezaji wa Etoile,”alisema Hans Poppe.
Kwa hisani ya Bin Zubeiry

No comments:

Post a Comment