Pages

Sunday, December 1, 2013

KOCHA MPYA SIMBA AWASILI NA KUKAGUA UWANJA WA KINESI, APOKELEWA NA MASHABIKI KIBAO






KOCHA mpya wa Simba Zdravko Logarusic amewasili nchini majira ya 2:15 asubuhi na Kenya Airways jana huku akitoa ahadi kemkem kwa mashabiki wa klabu hiyo yenye makao makuu mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam.

Logarusic raia wa Croatia ambaye awali alikuwa anaifundisha Gor Mahia ya Kenya na kuisaidia kuchukua Ubingwa baada ya ukame wa miaka 18 amesema yeye falsafa yake ni  ya kucheza mpira wa kushambulia haraka wakitokea nyuma (Counter attack) kwani ndio wenye kuleta matokeo mazuri.

Akizungumza baada ya kuwasili Logarusic ambaye anatarajia kusaini mkataba wa miezi sita leo amesema kuwa hatafanya mabadiliko ya wachezaji katika kikosi hicho zaidi ya kuhakikisha Simba inachukua ubingwa kama alivyofanya kwa Gor Mahia.

“Mimi kazi yangu ni kujenga timu ili icheze mchezo wa ushindani wenye kuonekana bayana hasa kufanya mashambulizi  ya haraka kwani nategemea Simba itabadilika na kutwaa ubingwa ili icheze kombe la mabingwa barani Afrika”, alijigamba Logarusic kocha nayeonekana kuwa muongeaji sana.

Kocha huyo amefikia Rombo View hotel iliyoko Shekilango, Urafiki  ambako amefikia golikipa Yaw Berko aliyesajiliwa na Simba kwa mkataba wa miezi sita kuitumikia Simba katika mzunguko wa pili wa ligi Kuu Tanzania bara.

Mara baada ya kufika hotelini na kupewa chumba na kupata kifungua kinywa alikwenda moja kwa moja kukagua uwanja wa Kinesi ambao unatumiwa na Simba kufanyia mazoezi na kuridhika nao japo alionekana kutaka kupata uwanja mwingine ambao anautumia anapokaribia kuwa na mechi.
Pia ametoa mapendekezo ya kupata mechi ya kirafiki kila wiki ili aweze kujenga timu yake katika ushindani wakati wote.

Kocha huyo alipokelewa na wajumbe watatu wa kamati ya Utendaji wa klabu ya Simba wakiongozwa na Saleh Pamba, Swedy Nkwabi na Damian Manembe na mashabiki waliokuwa kwenye Coaster tatu.

Logarusic amewahi kuzifundisha timu za King Faisal Babies FC Kumasi toka mwaka 2009/2010 na  Ashanti Gold SC toka 2010 hadi 2012 zote za nchini  Ghana na baadae alichukuliwa na Gor Mahia ya Kenya toka  Aprili 2012 hadi Novemba 2013.

No comments:

Post a Comment