Pages

Wednesday, December 4, 2013

KILIMANJARO STARS YATINGA ROBO FAINALI LEO KUCHEZA NA UGANDA

Na Mahmoud Zubeiry, Nakuru
TANZANIA Bara, Kilimanjaro Stars imefanikiwa kuingia Robo Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya kuifuga Burundi bao 1-0.
Bao pekee la Stars leo limefungwa na Mbwana Ally Samatta kwa kichwa dakika ya saba tu ya mchezo huo, akiunganisha krosi maridadi ya mshambuliaji mwenzake wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu.
Stars ingeweza kuondoka na ushindi mkubwa zaidi kama si uhodari wa kipa kinda wa Burundi, Arakaze Arthur aliyeokoa michomo mingi ya hatari.
Mbwana Samatta akiinua mikono kuwapungia mashabiki wachache Uwanja wa Afaraha leo baada ya mechi. Chini, Samatta akimtoka beki wa Burundi, Ndikumana Yussuf katika mechi hiyo.

Kwa matokeo hayo, Stars inayofundishwa na kocha Mdenmark, Kim Poulsen imemaliza na pointi saba, baada ya awali kushinda 1-0 dhidi ya Somalia na kutoa sare ya bila kufungana na Zambia.
Nani ataongoza kundi B- itajulikana baada ya mechi ya pili ya kundi hilo baina ya Somalia na Zambia inayoanza muda huu katika Uwanja wa Afrah pia.
Hadi sasa, Tanzania Bara na Zambia zinalingana kwa kila kitu na iwapo Chipolopolo itaifunga zaidi ya mabao mawili Somalia, ndiyo itaongoza Kundi na maana yake sasa, Stars itakutana na mabingwa watetezi, Uganda, The Cranes katika Robo Fainali.  
Iwapo Stars itakutana na The Cranes yenye wachezaji nyota kama Emmanuel Okwi aliyewahi kuchezea Simba na Hamisi Kiiza anayechezea Yanga za Dar es Salaam, itakuwa nafasi nzuri kwao kulipa kisasi cha kufungwa 3-0 mwaka katika Nusu Fainali mjini Kampala, Uganda. 
Lakini kama Stars itaongoza Kundi B, itakutana na Rwanda inayoongozwa na Nahodha, Haruna Niyonzima wa Yanga SC ya Dar es Salaam.  
Tanzania Bara; Ivo Mapunda, Himid Mao, Erasto Nyoni, Said Morad, Kevin Yondan, Frank Domayo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Amri Kiemba/Haroun Chanongo dk77, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta na Mrisho Ngassa/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk81. 
Burundi; Arakaza Arthur, Hakizimana Hassan/Abdulrazack Fiston dk81, Hererimana Rashid, Hakizimana Issa, Nsabiyumva Frederic, Nduwimana Jean, Ndikumana Yussuf, Duhayinavyi Gael/Mussa Mosi, Nduwarugira Christophe, Habonimana Celestin na Hussein Shaaban/Ndarusanze Claude. 

Kwa hisani ya Bin Zubeiry

No comments:

Post a Comment