Pages

Sunday, November 24, 2013

TAREFA YAOMBA USHIRIKIANO WA KUISAIDIA POLISI TABORA

CHAMA cha Soka Mkoa wa Tabora, (TAREFA) kimelitaka jeshi la Polisi Makao Makuu na Mkoa wa Tabora kuwapa ushirikiano wa kutosha ili  kuisadia timu ya Polisi Tabora kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu ujao.

Akizungumza kwa njia ya simu akiwa Tabora Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Tabora, (TAREFA) Yusuph Kitumbo amesema kuwa nguvu ya pamoja inahitajika ili kuhakikisha Polisi Tabora inapanda ligi kuu kwani imecheza daraja la kwanza bila kupanda kwa kipindi kirefu.

“Polisi Tabora inahitajika nguvu ya pamoja toka Makao Makuu ya Polisi, Mkoa na sisi chama cha soka ili kuisaidia timu ipande daraja kwani ipo nafasi ya tatu ikiwa ina pointi 12 kwenye kundi C hivyo tukishikamana pamoja timu itapanda kwani  ina wachezaji wazuri japo inakabiliwa na matatizo ya kiuchumi na vifaa”, alisema Kitumbo

Kitumbo alifika mbali na kusema wameamua kufikia maamuzi hayo kwani Poli ndio wamiliki wa timu hiyo hivyo wanapaswa kujua ushirikiano ni muhimu kuliko ilivyo sasa kwani wachezaji wanasafiri kwa kutumia ‘pick up’ kitu ambacho si vema kwa mchezaji kusafiri kwa magari ya wazi.

“Mchezaji anapaswa alipwe mshahara kwa wakati, apewe vifaa na akae mahali pazuri nikiwa na maana ya malazi na usafiri ili afanye kazi yake vema akiwa uwanjani, hivyo nawapongeza wachezaji kwa uvumilivu hadi hatua waliyofikia”, alisema Kitumbo


Polisi Tabora inafundishwa na Kocha Mwinyimad Tambaza ina pointi 12 nyuma ya JKT Kanembwa yenye pointi 12 ila zikitofautiana kwa mabao ya kufungwa na kufunga huku Stand United ikiongoza kundi C ikiwa na pointi 13.

No comments:

Post a Comment