Pages

Monday, November 25, 2013

KILIMANJARO STARS YAAGWA LEO, WACHEZAJI WAAHIDI MAKUBWA


Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa Henry Lihaya,(kulia) akipeana mkono na kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen kwenye hafla kukabimkabidhi bendera kwa Kilimanjaro Stars inayokwenda kushiriki mashindano ya Chalenji yanayotarajiwa kuanza kesho nchini Kenya. Katikati ni nahodha wa Kilimanjaro Stars Kelvin Yondani. 

Wachezaaji wa Kilimanjaro stars





Kikosi cha Kilimanjaro Stars imeagwa leo tayari kwa safari ya Nairobi, Kenya kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoanza kutimua vumbi Novemba 27 mwaka huu.

Hafla ya kuiaga timu hiyo imefanyika saa 5 asubuhi kambini kwao katika hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam. Msafara wa Kilimanjaro Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager unaongozwa na Ahmed Idd Mgoyi. Timu itaondoka saa 10 alasiri kwa ndege ya RwandAir.

Wachezaji waliomo katika msafara huo ni makipa Deogratius Munishi (Yanga), Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Michael Pius (Ruvu Shooting) na Said Moradi (Azam).

Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Ramadhan Singano (Simba) na Salum Abubakar (Azam).

Safu ya ushambuliaji inaundwa na Elias Maguli (Ruvu Shooting), Faridi Musa (Azam), Joseph Kimwaga (Azam), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngasa (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC).

Hata hivyo, washambuliaji Samata na Ulimwengu watajiunga na timu hiyo jijini Nairobi, Desemba Mosi mwaka huu wakitokea Lubumbashi ambapo Novemba 30 mwaka huu TP Mazembe itacheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Benchi la Ufundi la timu hiyo linawajumuisha Kim Poulsen (Kocha Mkuu), Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa Makipa), Leopold Tasso (Meneja wa Timu), Dk Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa Timu), Frank Mhonda (mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza Vifaa).

Kilimanjaro Stars ambayo ipo kundi B katika michuano hiyo itacheza mechi yake ya kwanza Novemba 28 mwaka dhidi ya Zambia kwenye Uwanja wa Machakos.

No comments:

Post a Comment