Pages

Tuesday, October 8, 2013

KAMATI YA JAJI LUANDA KUSIKILIZA RUFANI ALHAMISI

Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bernard Luanda itakutana keshokutwa (Oktoba 10 mwaka huu) kusikiliza rufani zilizowasilishwa mbele yake.

Waombaji uongozi watatu wamekata rufani katika Kamati ya Jaji Luanda wakipinga kutopitishwa kugombea katika uchaguzi wa TFF, uamuzi uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa ajili ya uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba 27 mwaka huu.

Warufani ni Samwel Nyalla aliyeondolewa kugombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda namba 2 ya mikoa ya Mara na Mwanza kwa kutojaza kikamilifu fomu namba 1 ya maombi ya kugombea uongozi TFF kwa kutoonesha malengo yake.

Ayoub Nyaulingo yeye anapinga kuondolewa kugombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda namba 6 (Katavi na Rukwa) kwa kutokuwa na uzoefu uliothibitika wa miaka mitano katika uongozi wa mpira wa miguu.

Naye Ayoub Nyenzi amekata rufani kupinga kuondolewa kugombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha Kanda namba 7 (Iringa na Mbeya) kwa kushindwa kuthibitisha uraia wake.

No comments:

Post a Comment