MANCHESTER, England
KOCHA wa Manchester United, David Moyes ameshikwa na
‘kitete’ juu ya ubora wa kikosi chake baada ya timu hiyo kupigwa mabao 2-1 na West
Bromwich Albion, Old Trafford kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, juzi.
Man United imeweka rekodi mbaya zaidi ya mwanzo wa ligi
katika kipindi cha miaka 24, kikosi cha Moyes kimefungwa mechi tatu kati ya
sita na kufanikiwa kupata pointi saba tu mpaka sasa na hii ni rekodi mbovu
zaidi ya United tangu msimu wa 1989-90, zama za mwanzo za Sir Alex Ferguson.
Moyes ameonyesha kuwa na hofu ya kushindwa kufanya vizuri
kwenye michuano ya Klabu Bingwa Ulaya, kutokana na kikosi chake kukosa
wachezaji wa kiwango cha dunia wa kutosha.
“Kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya, unahitaji wachezaji watano
au sita wa kiwango cha dunia,” alisema Moyes.
“Angalia Bayern Munich, wanajaa. Angalia Barcelona, walikuwa
nao siku za nyuma na Real Madrid,
ambao wanaweza kuwa nao sasa. Hivyo ndivyo unatakiwa kuwa kama
unataka kuchukua taji la Ulaya. Hatuna hilo
bado, lakini tumejaza uzoefu.
“Nilipopewa kazi hii, ilikuwa lazima mabadiliko yafanyike na
tukomae kadri siku zinavyozidi kusonga mbele.”
Moyes amekuwa na wiki ngumu baada ya Man United kufungwa
mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu England
na Manchester City
na West Brom na kocha huyo wa United amekiri kwamba matokeo ya timu hiyo
yanamtisha, hasa kutokana na timu hiyo kushindwa kufunga mabao ya ‘muvu’ kwenye
ligi tangu baada ya mechi ya Swansea.
“Yalikuwa matokeo mabovu na kiwango kibovu,” alisema Moyes,
“Hatukuonyesha mchezo mzuri. Tulimiliki mpira sana kipindi cha kwanza, lakini nafasi
hatukutengeneza. Na tulipozitengeneza hatukuzitumia. Walikuwa hatari zaidi
kwenye mashambulizi ya kushtukiza katika kipindi cha kwanza na zaidi walitisha
kipindi cha pili.
“Ndio ninahofu baada ya matokeo ya leo, lakini kwa sababu tu
hatukucheza vizuri. Kuna mechi nyingi zinakuja, nitajaribu na kuweka mambo sawa
kwenye mechi zijazo.”
Moyes aliongeza kwamba, kinachowaangusha ni kushindwa
kutengeneza mabao ya muvu na siyo kwamba hawana washambuliaji au wameshindwa
kuonyesha kiwango, anaamini kwamba wanahitaji kujituma zaidi.
Mskochi huyo alisema kwamba, kwenye mechi dhidi ya West
Brom, wachezaji walikuwa hawana hamasa uwanjani na walistahili kufungwa
kutokana na hilo.
United juzi ililala kwa mabao ya Morgan Amalfitano na Saido
Berahino, huku bao pekee la Man United likifungwa na Wayne Rooney kwa njia ya
adhabu.
@@@@
Mourinho
alia na Vertonghen
LONDON, England
KOCHA wa Chelsea, Jose Mourinho amemuangushia zigo la lawama
beki wa Tottenham Hotspur, Jan Vertonghen kwa kumtafutia kadi nyekundu straika
wake, Fernando Torres.
Katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, Mourinho
anaamini kwamba, Vertonghen alimdanganya mwamuzi na kumtafutia Torres kadi ya
pili ya njano na kusababisha straika huyo atolewe kwa kadi nyekundu.
“Timu yangu ilikuwa vizuri sana,
mpaka mwamuzi alipofanya makosa, makosa makubwa ambayo yalichangia sana kusababisha matokeo
yawe vile. Mwamuzi hana hatia, Mchezaji (Vertonghen) ndiye mwenye hatia.
Alijidanganyisha kana kwamba ameguswa sana
na Fernando (Torres) na mwamuzi akamuamini na kutoa kadi,” alisema Mourinho.
Mourinho anaamini kadi hiyo ya Torres aliyoipata zikiwa
zimesalia dakika 10 mechi kuisha, kwa kiasi kikubwa iliinyima ushindi timu
yake, ambayo ilikuwa ikishambulia kwa kasi wakati huo.
@@@@
Arsenal, Liverpool zamnyatia Balotelli
LONDON, England
ARSENAL na Liverpool zinaangalia uwezekano wa kumsajili
straika mtukutu wa AC Milan,
Mario Balotelli wakati wa dirisha dogo la usajili la Januari.
Kumekuwa na taarifa nchini Italia kwamba, Balotelli ‘Mad
Mario’ tangu alipoondoka Manchester
City amekuwa na vipindi
tofauti akiwa AC Milan.
Pia amekuwa akikutana na tatizo la ubaguzi wa rangi kila kukicha
kwenye majukwaa ya soka ya Italia, hivyo wachambuzi wa mambo wameanza kuamini
kwamba kunauwezekano wa straika huyo kuuzwa kwa dau la pauni milioni 12 na
Arsenal na Liverpool zinaweza kumtupia ndoano.
No comments:
Post a Comment