Pages

Friday, August 16, 2013

KIVUMBI LIGI KUU ENGLAND, MATARAJIO, UTABIRI WA TIMU 20 SHIRIKI


LIGI Kuu England msimu wa 2013-14, inaanza kutimua vumbi kesho kwenye viwanja mbalimbali nchini humo.
Kila klabu inahaha kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu mpya na kutengeneza mazingira mazuri ya kupata mafanikio.
LENZI YA MICHEZO inakuletea uchambuzi wa kina kuhusu klabu zote 20 zitakazoshiriki ligi hiyo msimu huu.

Arsenal: Msimu uliopita; 4, matarajio: Top 4, utabiri; 4
The Gunners wamekuwa kimya kwenye dirisha la usajili, licha ya taarifa fedha ipo, wana pauni milioni 80 mfukoni, Arsene Wenger mpaka sasa amemnasa Yaya Sanogo pekee, tena bure. Amewakosa kina Gonzalo Higuain na Stevan Jovetic kutokana na ubahili wake. Kwa sasa wanahaha kumsaka Luis Suarez.
Hakuna mbadala wengi sokoni, wanatakiwa kutoa pauni milioni 50 kumnasa Suarez, swali je, Wenger atatoa? Wanakila kitu kinachoweza kuwapa mafanikio kwenye ligi, lakini wanakosa straika wa kufunga mabao zaidi ya 25 kwa msimu. Wameitema mizigo kama kina Marouane Chamakh, Gervinho, Denilson, Sebastien Squillaci na  Andre Santos na kuna wengine wanafuata.
Mchezaji muhimu: Santi Cazorla ndiyo injini kwenye kiungo cha timu hiyo na mchezeshaji wa mastraika.

Aston Villa; Msimu uliopita: 15, matarajio: Kuepuka kushuka daraja, utabiri: 13
Kocha Paul Lambert alitegemea zaidi vijana kuikoa timu kushuka na alifanikiwa, sasa baada ya kupata uzoefu wa mwaka mmoja, wanatarajiwa kufanya vizuri msimu ujao. Kumbakiza Christian Benteke ilikuwa lazima. Beki yao inatakiwa kuboreshwa wamesajili beki kutoka Sevilla Antonio Luna na Jores Okore, wakiungana na Nathan Baker na Matt Lowton watakuwa vizuri zaidi.
Mchezaji muhimu: Christian Benteke, ndiye ataongeza mashambulizi yao.

Cardiff City: Msimu uliopita: Wamepanda, matarajio: Kuepuka kushuka daraja; Utabiri: 18
Malky Mackay amefanya jambo la busara kutambua sehemu za kuimarisha kwenye timu yake, kubaki ligi kuu kutategemea vitu viwili, kiwango cha nyumbani na rekodi ya mabeki. Kumsajili Steven Caulker kutoka Tottenham, kutawasaidia kuwa na beki nzuri. Ujio wa John Brayford kutoka Derby, utaongeza nguvu nyuma. Mabao yanahitajika na uwepo wa Frazier Campbell na Nicky Maynard utawabeba idara hiyo, pia usajili wa Andreas Cornellius kutoka Copenhagen ni biashara nzuri.
Mchezaji muhimu: Kombinesheni ya Peter Whittingham na Craig Bellamy itakuwa muhimu.

Chelsea; Msimu uliopita: 3, matarajio: Ubingwa, utabiri; 1
Mpaka sasa Chelsea ndio timu bora ligi kuu, The Blues kwa sasa wameungana tena na Jose Mourinho ambaye ataifanya timu yake iwe tayari kwa mapambano toka siku ya kwanza. Hawajafanya usajili mkubwa sana, lakini wanakikosi kikubwa. Wamemnasa Andre Schurrle kutoka Bayer Leverkusen na Marco van Ginkel kutoka Uholanzi.
Fernando Torres na Demba Ba kidogo uwezo wao unatia shaka, Mourinho atasajili straika mwingine. Wayne Rooney atawapa kitu wanataka. Utatu mtakatifu wa Juan Mata, Oscar na Eden Hazard utatisha na wakiwa na Mourinho wapinzani watakoma.
Mchezaji muhimu: Romelu Lukaku ndiye anaweza kuwa straika namba moja Chelsea kwa sasa.

Crystal Palace: Msimu uliopita: Wamepanda, matarajio: Kuepuka kushuka daraja, utabiri: 20.
Pamoja na kwamba Ian Holloway ni bonge la kocha, kikosi chake hakina ubora wa kubaki ligi kuu, kitendo cha kushindwa kumbakiza Wilfried Zaha kwa mkopo tena kutoka Manchester United, kutaathiri safu yao ya ushambuliaji. Usajili Dwight Gayle kutoka Peterborough, hauwezi kuziba pengo lake.
Mchezaji muhimu: Yannick Bolasie atalazimika kuongeza ufundi ambao umepotea baada ya kuondoka kwa Zaha.

Everton: Msimu uliopita: 6, matarajio: Top 6, utabiri: 8
Everton ilipokuwa chini ya David Moyes ilikuwa haitetereki, lakini sasa ameondoka na mikoba yake imechukuliwa na Roberto Martinez, ambaye wachambuzi wa soka wanahofu kama anaweza kuipaisha timu hiyo. Hawajapoteza wachezaji wengi wakati huu wa kiangazi zaidi ya kumuongeza Arouna Kone ambaye atacheza sambamba na Nikica Jelavic na kuiongeza nguvu safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Usajili wa mkopo wa Gerard Deulofeu kutoka Barcelona, watu wanasubiri kuona akikomaa atakuaje kwa sababu ni mmoja kati ya vipaji vya kweli kutoka La Masia, atapata nafasi ya kucheza. Ni winga anayeweza kucheza kulia na kushoto.
Mchezaji muhimu: Marouane Fellaini na Leighton Baines, ndio watakuwa injini ya timu.

Fulham: Msimu uliopita: 12, matarajio: Top 10, utabiri: 16
Fulham hawatakuwa na msimu mzuri na wanahati hati ya kuwa miongoni mwa timu zitakazokuwa zinapigana kuepuka kushuka daraja. Licha ya kufanya usajili mpya kwa kuwaleta watu kama kina Fernando Amorebieta, Derek Boateng na Maarten Stekelenberg, umri mkubwa wa wachezaji wake unaweza kuwafanya wakachemka, pia hawana mbadala kwenye safu yake ya ushambuliaji. Adel Taarabt ataongeza ubunifu baada ya kutua kwenye timu hiyo kwa mkopo.
Mchezaji muhimu: Dimitar Berbatov anahitaji kuendelea kufunga msimu huu na mabao 15 yatatosha kuwaokoa wasishuke daraja.

Hull City: Msimu uliopita: Wamepanda, matarajio: Kuepuka kushuka daraja, utabiri: 19
Steve Bruce ameiongoza Hull kupanda daraja msimu uliopita, timu hii inaweza kuwa nzuri nyuma na kucheza mechi kadhaa bila kuruhusu bao, lakini kitakachoiharibia ni kukosa safu kali ya ushambuliaji. Danny Graham anawapa nafasi ya kupambana, usajili mpya Yannick Sagbo bado hajathibitisha uwezo wake.
Mchezaji muhimu: Sone Aluko na Ahmed Elmohamady, wanahitaji kuwalisha Sagbo na Graham kama wanataka kubaki Ligi Kuu.

Liverpool: Msimu uliopita: 7, matarajio: Top 6, utabiri: 7
Brendan Rodgers anajitahidi kutengeneza timu ya ushindi Liverpool. Usajili wake wa Januari, Phillipe Coutinho ulikuwa bora. Wakati huu Luis Suarez akitarajiwa kuondoka, majukumu ya kufunga yako mikononi kwa Daniel Sturridge na Fabio Borini, wachezaji wapya pia Iago Aspas na Luis Alberto, wanahitaji kufanya makubwa kwenye msimu wao wa kwanza klabuni, Kolo Toure ametua bure kuchukua mikoba ya Jamie Carragher.
Mchezaji muhimu: Phillipe Coutinho anahitaji kuwa kwenye kiwango cha juu sana ili timu ifanye vizuri.

Manchester City: Msimu uliopita: 2, matarajio: Ubingwa, utabiri: 2
Kocha mpya Manuel Pellegrini anahitaji kuvaa viatu vya Roberto Mancini mapema, baada ya kutumia zaidi ya pauni milioni 100 kwenye usajili wakati huu wa kiangazi, matarajio ya wengi ni City kuwa mabingwa na kufika mbali Ulaya. Kuchukua nafasi ya Carlos Tevez, amesajiliwa Stevan Jovetic na Jesus Navas, anatarajia kuongeza ubunifu kwenye kiungo cha timu hiyo.
David Silva alionekana kuchoka msimu uliopita, ujio wa Navas utamuibua upya. Fernandinho atacheza sambamba na Yaya Toure na kuimarisha kiungo cha timu. City wanahitaji kuimarisha beki yao.
Mchezaji muhimu: Sergio Aguero anahitaji kurudi kwenye fomu msimu huu na kufunga mara kwa mara kama kweli City inataka kufanya vizuri msimu huu.

Manchester United: Msimu uliopita: 1, matarajio: Mabingwa, utabiri: 3
Kocha mpya, David Moyes ameshindwa kufanya usajili wa mchezaji mwenye jina kubwa mpaka sasa, kukosekana kwa wachezaji wapya kunaweza kuwanyima ubingwa. Wapinzani wao wakubwa mbio za ubingwa ni Manchester City na Chelsea na wote wamefanya usajili mkubwa hasa kwenye eneo la kiungo, ili kuivua United ubingwa. Ukiangalia vikosi vyao na kulinganisha na Man United, unaona kwamba United hawana kiungo kikubwa. Michael Carrack ndiye bora eneo hilo.
Wanakosa ubunifu na waliwakosa mafundi Lucas Moura na Eden Hazard katika miaka ya karibuni. Beki na safu yao ya ushambuliaji, inaweza kuchuana na City na Chelsea, sasa wanahitaji kuvunja benki kwa ajili ya kiungo wa kiwango cha kimataifa, mtu kama David Silva au Juan Mata, na kama wakimpata mtu watachuana nao.
Mchezaji muhimu: Robin van Persie ataongoza mashambulizi ya Man United.

Newcastle United: Msimu uliopita: 16, matarajio: Top 10, utabiri: 9
Lengo lao kuu wakati huu wa kiangazi ilikuwa ni kutafuta mtu wa kuchukua nafasi ya Demba Ba, ambaye Januari wamefanya hilo kwa kumnasa Loic Remy kwa mkopo kutoka QPR, Remy ni chaguo sahihi la kumuongezea nguvu Papiss Cisse. Msimu uliopita kilichowaharibia ni kukosa kikosi kikubwa.
Mchezaji muhimu: Hatem Ben Arfa kama akiwa fiti kwa sehemu kubwa ya msimu, timu hiyo itafika mbali.

Norwich City: Msimu uliopita: 11, matarajio: Katikati, utabiri: 11
Chris Hughton anajua nini anatakiwa kufanya msimu huu ili Norwich wasonge mbele na ameshawaleta wachezaji wenye vipaji kama kina Ricky van Wolfswinkel na Gary Hooper, pia kumsajili moja kwa moja Javier Garrido ni jambo sahihi alikuwa beki wao bora msimu uliopita na ujio wa Leroy Fer kwenye kiungo umeongeza nguvu kwenye timu.
Mchezaji muhimu: Gary Hooper ndiye muhimu zaidi Norwich.

Southampton: Msimu uliopita: 14, matarajio: Katikati, utabiri: 12
Mauricio Pochettino ataifundisha Southampton toka mwanzo wa msimu na ameshasajili aina ya wachezaji anaowapenda, amewaleta kina Victor Wanyama na Dejan Lovren. Hawa wote ni viungo wa ulinzi, Wanyama anaweza kucheza pia kama beki wa kati.
Wanahitaji kusajili mshambuliaji mwingine kumuongezea nguvu, Ricky Lambert na Jay Rodriguez.
Mchezaji muhimu: Gaston Ramirez bado hajathibitisha ubora wake tangu alipotua kwenye timu hiyo kutoka Bologna.

Stoke City: Msimu uliopita: 13, matarajio: Katikati, utabiri 17
Stoke wako hatarini kushuka daraja, wameshindwa kusajili wachezaji wa ukweli. Kuondoka kwa Tony Pulis ni pigo kubwa kutokana na kocha huyo kuwa ameshatengeneza timu yake na anaijua vilivyo. Stoke itakutwa na majanga kama yaliyowakuta Charlton, baada ya kuondoka Alan Curbishley. Mark Hughes ameingia kwenye timu na hajafanya usajili wa maana zaidi ya kumleta Erik Pieters kutoka PSV.
Mchezaji muhimu: Charlie Adam anatakiwa kutawala kiungo cha timu hiyo na kumlisha Peter Crouch zaidi.

Sunderland: Msimu uliopita: 17, matarajio: Katikati, utabiri: 14
Paolo Di Canio amekuwa akifanya biashara zake kimya kimya, akimleta Jozy Altidore kutoka AZ Alkmaar, wakati huu wa kiangazi acheze sambamba na Steven Fletcher. Sunderland walikuwa wabovu nyuma hivyo wamesajili Modibo Diakite bure kutoka Lazio. Pia usajili wa Emanuele Giaccherini kutoka Juventus utaongeza ubunifu.
Mchezaji muhimu: Jozy Altidore anahitaji kufunga kila wiki kuipa matumaini ya kufanya vizuri timu hiyo.

Swansea City: Msimu uliopita: 9, matarajio: Top 8, utabiri: 6
Michael Laudrup anatengeneza kikosi kikali Swansea kwa ajili ya michuano ya Ulaya. Kuchukua Kombe la Ligi na kumaliza nafasi ya tisa siyo jambo la kubeza. Hawajapoteza wachezaji wao muhimu, wamembakiza Michu na jeshi lake. Wamesajili wachezaji wengine wakali mapema.
Wilfried Bony alikuwa balaa msimu uliopita Uholanzi, akifunga mabao 31 msimu uliopita, amesajiliwa kwa dau la pauni milioni 12. Michu anaweza kucheza nyuma ya Bony. Jonjo Shelvey yuko vizuri pia.
Mchezaji muhimu: Kombinesheni ya Michu na Bony itakuwa ndiyo siri ya mafanikio ya klabu msimu ujao.

Tottenham Hotspur: Msimu uliopita: 5, matarajio: Top 4, utabiri: 5
Spurs wamekosa kidogo tu kushiriki ligi ya mabingwa kwa misimu miwili nyuma. Kutetereka nusu ya pili ya msimu ndiyo tatizo lao kubwa. Wamefanya bonge la usajili wakati wa kiangazi, Paulinho ameongeza nguvu kwenye kiungo na atacheza sambamba na Sandro, Nacer Chadli ataongeza nguvu kwa Gareth Bale kama akibaki. Bale wakibaki wana nafasi ya kumaliza Top 4, lakini bahati mbaya ni lazima aondoke, Roberto Soldado ni bonge la straika anayeweza kufunga mabao zaidi ya 30 kwa msimu.
Mchezaji muhimu: Roberto Soldado atahitaji kufunga kila wiki kama wanataka kumaliza Top 4.

West Brom: Msimu uliopita; 8, matarajio: Katikati, utabiri: 15
Jamaa msimu uliopita walivuka malengo na kumaliza nafasi ya nane, lakini kuondoka kwa Romelu Lukaku aliyerudi Chelsea ni pigo, Nicolas Anelka amekuja, lakini ubora wake unatia shaka kama uko kama zamani, usajili wa Diego Lugano utaongeza nguvu kwenye beki ya timu hiyo.
Mchezaji muhimu: Shane Long anahitaji kuwa fiti na kuziba pengo la Lukaku.

West Ham: Msimu uliopita: 10, matarajio  Top 10, matarajio: 10
Sam Allardyce amehakikisha mastaa wake wote wamebaki, Mohamed Diame, Mark Noble na James Tomkins wamebaki klabuni. Wamemleta Andy Carroll kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, baada ya kuichezea kwa mkopo timu hiyo msimu uliopita, usajili wa Stewart Downing utaongeza nguvu pembeni.
Mchezaji muhimu: Andy Carroll amesajili kwa pauni milioni 15 na atatakiwa kuthibitisha thamani yake kwa kucheka na nyavu.


No comments:

Post a Comment