DALILI zinaonyesha kuwa siku za Wayne Rooney zinahesabika.
Maswali kama ataondoka? Atabaki? Kweli anataka kuondoka! Siku zote hutoa dalili
kwamba, maisha ya mchezaji kwenye klabu husika yamefika tamati.
Kwenye soka lolote linaweza kutokea, siku za mtu ndani ya
klabu zinaisha siku yoyote, kama huamini waulize makocha waliowahi kuifundisha
Chelsea katika zama za Roman Abramovich.
Hata hivyo kwa ishu ya Rooney, madai ya kutaka kuhama
yanaonyesha pasipo na shaka yoyote kwamba, siku zake ndani ya Old Trafford
zimeisha.
Makala haya yanaangalia sababu tano ambazo zinaonyesha wazi
kuwa, Rooney anaondoka Old Trafford na mchezaji yeyote akikutana na sababu hizi
ujue siku zake kwenye klabu zimeisha.
Kuondoa jina muajiri
kwenye akaunti yake ya Twitter
Mei mwaka huu wakati sakata hili la Rooney kutuma maombi ya
kuondoka Man United likiwa bado jipya kabisa, Rooney kwa mshangao wa wengi
aliamua kutoa jina la Manchester United, kwenye akaunti yake ya Twitter.
Ni uamuzi mkubwa sana kuamua kubadilisha maneno kwenye jina
lililopo katika akaunti ya Twitter. Kwenye twitter mtu hupewa maneno herufi 160
kujielezea jina lako kwenye akaunti yako.
Lakini, Rooney kwa mshangao wa wengi, alifuta jina la
Manchester United player (Mchezaji wa Manchester United) na kuweka, @NikeUK
athlete (@Mwanamichezo wa NikeUK).
Hii inamaanisha kwamba, ukiingia kwenye akaunti ya twitter
ya Rooney sasa hivi, huwezi kujua anachezea timu gani.
Kinachoweza kukusaidia ni picha yake kwenye akaunti hiyo
ambayo inamuonyesha akiwa amevaa jezi ya Man United. Au ukiingia kwenye mtandao
wake binafsi na kumuona akiwa na picha nyingi ambazo amevaa jezi za Man United,
mbali na hayo hakuna kingine kinachoonyesha anachezea klabu gani.
Kuzomewa na mashabiki
kwenye gwaride la ubingwa
Pale furaha ya mashabiki wa klabu wanapokuwa wakisherehekea
ubingwa wao wa kihistoria wa 20, inapokatishwa na chuki dhidi ya mchezaji, hapo
ujue kuna tatizo.
Wakati mashabiki wa Man United wakiwa kwenye sherehe za
gwaride la ushindi wa Ligi Kuu England, Mei mwaka huu, walikatisha sherehe yao
kwa muda na kumzomea, Rooney ambaye alistahili pongezi kutokana na kuchangia
kupatikana kwa ushindi huo kutokana na mabao yake 12 aliyofunga na kupiga pasi
za mwisho 10 kwenye mechi 27.
Inauma kuzomewa na mashabiki wa timu yako, lakini inauma
zaidi unapozomewa wakati wa hafla ya ushindi, hiyo ni dalili tosha kwamba, muda
wa mchezaji kwenye ndani ya timu umeisha.
Pale mashabiki
waliolilia usajiliwe, wanasema ondoka
Jumatano, gazeti la Manchester Evening News, liliomba maoni
ya kijana ambaye mwaka 2004 akiwa na miaka 11, alibeba bango lililosema:
‘Please Buy Rooney’ (Tafadhali mnunue Rooney) na kuingia nalo Old Trafford.
‘Please Buy Rooney’ (Tafadhali mnunue Rooney) na kuingia nalo Old Trafford.
Sir Alex Ferguson, alifuata maoni ya mtoto huyo na kumsajili
Rooney muda mfupi mbele, lakini sasa hivi mtoto huyo ana miaka 20 na mtazamo
wake kuhusu Rooney umebadilika.
Joe Ruane, ambaye alilia Rooney kusajili mwaka 2004, safari
hii alipoulizwa kuhusu Rooney alitoa ushauri wa klabu hiyo kumuuza, huku akidai
hakuna mchezaji ambaye ni mkubwa kuliko klabu na kuongeza kuwa alimuona shujaa
lakini sasa hivi na aondoke zake.
Bifu la zamani na
kocha mpya
Siku za mchezaji ndani ya klabu zinaweza kuwa zinahesabika
pale, kocha mpya anapoingia kwenye klabu wakati amewahi kuwa na bifu na
mchezaji siku za nyuma.
Taarifa za ujio wa David Moyes, Old Trafford inaonekana
zilikuwa kama msumari wa moto kwa Rooney, kutokana na siku za nyuma kuwahi
kutofautiana na kocha huyo.
Moyes aliwahi kumshitaki Rooney kwa kumchafulia jina mwaka
2008, baada ya Rooney kumuandika vibaya kocha huyo kwenye kitabu chake cha
Wayne Rooney: My Story So Far, inasemekana Moyes alishinda kesi hiyo na kulipwa
na Rooney faini kati ya pauni 50,000 na 150,000.
Kutokana na zengwe hilo, Rooney mwenyewe anaweza kuona aibu
na kuamua kufungasha kilicho chake na kuondoka, japokuwa baada ya kesi hiyo,
Rooney alimuomba msamaha Moyes.
Kung’ang’ania kuhama
kila kukicha
Oktoba 2010, Rooney aliwasilisha maombi yake ya kwanza ya
kuondoka Old Trafford.
Septemba 2012, Rooney inasemekana aliingiwa na majuto sana
na kudai maombi yake ya kuhama lilikuwa ni moja ya kosa kubwa zaidi kwenye
maisha yake ya soka.
Mei 2013, kwa mujibu wa kocha wa zamani wa Man United, Sir
Alex Ferguson, Wayne Rooney aliomba tena kuondoka Man United.
Hii inamaanisha kwamba, majuto aliyokuwa nayo Septemba 2012,
yalikuwa yakinafiki.
Kuna muda mchezaji anaona dalili kuwa hatakiwi, kutoka kwa
kocha, mashabiki, mke na watoto, lakini kutuma dalili za mchezaji kuondoka
klabuni zinakuwa kubwa zaidi pale anapoanza kung’ang’ania kufanya hivyo.
Pale mchezaji anapong’ang’ania kuhama, basi ni wazi kuwa
ataondoka.
No comments:
Post a Comment