Pages

Thursday, August 1, 2013

BALE MKUBWA KULIKO SPURS, SASA AENDE ZAKE MADRID

GARETH Bale alipokea mpira akiwa upande wa kulia wa uwanja, akauhamishia kwenye guu lake la kushoto, akaingia nao ndani na kuachia shuti kali la umbali wa yadi 25, lililomshinda kipa wa Sunderland, Simon Mignolet.

Hilo ndilo bao la mwisho la Bale msimu uliopita, ambalo liliwapa matumaini ya muda ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Lakini ushindi wa bao 1-0 walioupata Arsenal dhidi ya Newcastle United kwenye uwanja wa St James' Park, ulikatisha ndoto na furaha pale White Hart Lane.

Bao hilo lilikuwa limepunguza presha ya kumbakiza Bale, White Hart Lane, kwa msimu mwingine kwa sababu lingeweza kuwapeleka ligi ya mabingwa, lakini ushindi wa Arsenal uliwabakiza nafasi ya nne, na Spurs wakarudi tena kwenye Europa League. Mafanikio ya Bale baada ya mechi hiyo yalikosa mashiko.
“Kila la kheri Hispania, Gareth (Bale),” mmoja wa mashabiki alisikika akisema wakati wachezaji wakiingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, tayari walihisi hili linakuja.

Hakuna ambaye anaweza kujua kama kumaliza nafasi ya nne kungembakiza Bale kwa msimu mwingine na kumshawishi kuongeza mwaka mmoja zaidi katika ile sita aliyokaa White Hart Lane.
Bale alifurahia sana kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2010-11, na kiwango chake dhidi ya timu za Milan kilimtambulisha kimataifa na kiwango chake huko ndicho kilianza kuzivuta klabu za Real Madrid na Inter Milan. Je, Bale angejawa na hisia za kipekee, kushuhudia usiku wa Ligi ya Mabingwa kwenye uwanja wa White Hart Lane tena?

Bahati mbaya kwa Spurs, Madrid ndio wanamtaka Bale na wako tayari kutoa zaidi ya pauni milioni 80, kwa ajili yake, kwa hiyo hata kama Spurs wangemaliza katika nafasi ya nne kumbakiza Bale, bado ingekuwa kazi sana, kwa sababu kama kucheza Ligi ya Mabingwa angeenda Celtic.
Lakini kilichopo hapa, Bale (24) anataka zaidi. Anataka kuona raha ya kucheza klabu kubwa, ambayo inaweza kuchuana kuwania mataji makubwa na kupata mafanikio zaidi ambayo Spurs hawawezi kumpa, hivyo ndoto zake zote ziko Santiago Bernabeu.

Aliizungumzia vizuri klabu hiyo kabla ya kukutana nao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, katika uwanja wa Bernabeu mwaka 2011, msimu ambao Spurs walishiriki michuano hiyo.
Je, Tottenham watambakiza? Hakuna ubishi kwamba wangependa kufanya hivyo na wako radhi kufanya lolote. Andre Villas-Boas alimpa Bale majukumu ya kucheza huru msimu uliopita, akicheza kama namba 10 na uhusiano kati ya AVB na Bale ni mkubwa. Wamekuwa marafiki wa karibu katika miezi 12 iliyopita.

Halafu kuna huyu Mwenyekiti, Daniel Levy, ambaye ni ngumu kusema kama yuko karibu na Bale. Amekataa kusikiliza ofa yoyote ya Bale, japokuwa anaweza kujikuta akilia siku za usoni. Kitendo cha kukataa kumuuza Luka Modric kwa dau la pauni milioni 40 misimu miwili iliyopita, inaonyesha jinsi gani anamaanisha anachokisema.

Aliwahi kuwaachia kwa mbinde, Dimitar Berbatov na Michael Carrick kwenda Manchester United na Modric kwenda Real Madrid.
Hapa kinachoangaliwa ni fedha na kufikia dau analolitaka Levy, kuliko maombi ya mchezaji kuhama na kwenda kwenye ushindani zaidi.

Alimlipia Bale pauni milioni 5 kutoka Southampton mwaka 2007, lakini ni wazi sasa hivi Bale amekuwa kuliko klabu na ni wakati wake kuondoka.
Kuna sababu tatu ambazo zinamuondoa Spurs, Bale aliyefunga mabao 21 kwenye Ligi msimu uliopita.

Kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya
Linapokuja suala la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Bale anauamuzi rahisi sana, kubaki Tottenham na kucheza Europa League na kusubiri msimu mwingine kusaka tiketi ya kushiriki michuano hiyo, au anaweza kujiunga na klabu ambayo imeshinda mara tisa michuano hiyo na inasaka taji la 10. Akiwa Real Madrid, itakuwa rahisi kwake kushiriki. Wakati huu ambao kiwango chake kiko juu, Bale anatakiwa kwenda Santiago Bernabeu na kuchezea klabu ambayo imefika nusu fainali tatu za ligi ya mabingwa katika misimu mitatu iliyopita. Badala ya kubaki kwenye timu ambayo pamoja na kufunga mabao mengi, imeshindwa kumaliza katika nafasi nne za juu England, anatakiwa kwenda Madrid na kuungana na Carlo Ancelotti, aliyeshinda taji hilo mara mbili.

Kukumbukwa milele
Akiwa kama staa wa Tottenham, Bale ameingia kwenye orodha ya mastaa wa Ligi Kuu England. Chelsea kuna Eden Hazard, Manchester United kuna Robin van Persie na Liverpool kuna Luis Suarez. Haya ni majina yanayoweza kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha dunia, lakini je, watakumbukwa baada ya miaka 10? 
Labda Van Persie; kutokana na kiwango chake kilichoipa ubingwa Man United, nani mwingine atakumbukwa? Wale ambao hawawezi kusahaulika ni wachezaji waliofanya vizuri kimataifa na siyo England tu, watu kama kina Cristiano Ronaldo, David Beckham, Lionel Messi, Zinedine Zidane na Ronaldinho. Hata Galacticos. Ndio ni wachezaji wachache sana ambao hawawezi kusahaulika na wengi wao wamechezea Real Madrid au Barcelona. Hivyo hii ni nafasi yake kwenda Hispania na kuandika historia, kwa nini abaki England?

Je, Bale atakuwa na subira kama Gerrard?
Ukimuuliza shabiki yeyote wa Spurs, jina gani linakuja akilini ikitajwa Tottenham Hotspur, kuna jina moja tu. Pale White Hart Lane, Bale anafanya kila kitu, lakini mpaka lini ataendelea kuwa hivi? Je, Bale anaweza kuwa jeshi la mtu mmoja mpaka akifikisha miaka 30? Au atabaki kwa misimu kadhaa kabla ya kuchoka? 

Japo ni ngumu kwa mashabiki wa Liverpool kukubali, lakini Steven Gerrard amefanya kila awezalo kuipa mafanikio timu hiyo, lakini amegonga ukuta. Gerrard ameibeba timu yake ya utotoni miaka nenda rudi bila taji la ligi kuu. Ndio pamoja na kukosa mataji, lakini nahodha huyo wa Liverpool amevuna heshima, utiifu na kuungwa mkono. Lakini je, hayo yatamtosha Bale? Siyo kila mchezaji anapata nafasi ya kujiunga na Real Madrid, na itashangaza kukataa ofa hiyo, ambayo itamuwezesha kufikia malengo yake.



No comments:

Post a Comment