Pages

Sunday, June 9, 2013

ARJEN ROBBEN NA PESA JUU; BIASHARA BOMU LIVERPOOL?

LIVERPOOL, England
BARCELONA, habari kuu kwenye jiji hilo ni usajili wa supastaa wa Brazil, Neymar, kujiunga na wakali wa La Liga, Barca. Uhamisho wa staa huyo kutoka Santos, ni kama sarafu yenye pande mbili zinazokinzana. Kuna upande una furaha hadi kupitiliza, lakini upande mwingine umekuwa na hofu kubwa.
Upande wa wenye wasiwasi ni kuhusu hali itakavyokuwa juu ya uhusiano baina ya Mbrazil huyo na Muargentina, Lionel Messi - wataishije mafahali hao wawili kwenye zizi moja la Nou Camp.
Jambo hilo limemshitua hadi gwiji la klabu hiyo, Johan Cruyff, aliliona hilo wiki chache zilizopita na alisema "huwezi kuwa na manahodha wawili wakiongoza meli moja". Kuna upande mwingine unaamini hakutakuwa na tatizo juu ya jambo hilo na kwamba usajili wake umewafurahisha kwa sababu utaifanya Barca kuwa imara zaidi.
Neymar - alisema kwamba ametua Barca kumsaidia Messi kuendelea kuwa mchezaji bora wa dunia. Lakini, kwa hali ya mambo ilivyo, kuna hofu kubwa kwamba wawili hao wataibua vita ya kutaka kufahamika nani mtawala nje ya uwanja. Wengi wanaamini kwenye hilo, halitamuhusu Messi peke yake, Barca ina wachezaji wengi wenye majina makubwa kwenye kikosi chao.
Lakini, sasa Neymar alikotoka, Santos alikuwa bosi na sasa amekwenda kwenye timu ambayo jambo hilo linaweza kuwa si tatizo kwa upande wake. Mahali hapa tatizo halitaanzishwa na Neymar - bali na Messi mwenyewe, kwa sababu atakuwa hana amani. Haya, tuliache hilo la Barca na Neymar wao.
Mjadala uliopo mezani kwa siku ya leo ni kuhusu mchakato wa Bayern Munich kutaka kumsajili mshambuliaji wa Liverpool, Luis Suarez. Na usajili wake utahusu ofa ya kwamba Bayern wapo tayari kumpeleka Arjen Robben pamoja na fedha juu ili kuipata saini ya mkali huyo wa Uruguay. Je, dili hili limetulia?
Ripoti zinabainisha kwamba Bayern inamtaka Suarez, na imejiandaa kumtoa Robben pamoja na fedha juu kama ofa ya kumnasa mkali huyo kutoka Amerika Kusini, ambaye ni mwingi wa vituko.
Suarez hivi karibuni alibainisha matakwa yake ya kutaka kuhama Anfield, huku jambo hilo likichagizwa na mashambulio ya vyombo vya habari dhidi yake, lakini huku kukiwa na taarifa kwamba Liverpool haitakuwa tayari kumruhusu staa wao huyo aondoke.
Kwa vyovyote itakavyokuwa, iwe kwa matakwa ya mchezaji au klabu yake, timu kubwa siku zote zitaendelea kufukuzia namna ya kuipata saini ya mchezaji husika. Na sasa Bayern inaonekana imeketi mbele kabisa katika foleni ya kumdaka mchezaji huyo, lakini kwa hali jinsi ilivyo, Liverpool wanaweza wasikubali ofa hiyo, hawataikubali.
Robben alitumia nafasi nzuri, wakati Toni Kroos alipopata majeraha ya misuli katika kikosi cha Bayern msimu uliopita, alijaribu kucheza kwa kiwango kikubwa na kujipenyeza kwenye kupata nafasi katika kikosi cha kwanza.
Na tangu hapo, Robben aliweza kupata nafasi ya kucheza katika mechi zote za Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, akifunga mabao muhimu, ikiwamo la ushindi kwenye mechi ya fainali dhidi ya Borussia Dortmund, kwenye Uwanja wa Wembley, London mwezi uliopita.
Aliboresha staili yake ya uchezaji, anapopata mpira alikuwa akifikiria kushambulia zaidi na jambo hilo lilimfanya kuwa kivutio katika kumtazama na hapo Robben akaonekana kuwa mchezaji aliyeibua upya ujuzi wake ndani ya uwanja.
Lakini, licha ya kuwa na kiwango bora kwa sasa, kocha mpya wa Bayern, Pep Guardiola, hatarajiwi kuendelea kumtumia Robben wakati atakapochukua rasmi mikoba ya kuinoa klabu hiyo yenye maskani yake Allianz Arena.
Mabosi wa Bayern wataendelea kusaka wachezaji wenye hadhi za kuwapo kwenye kikosi chao, lakini kwa Liverpool, sidhani kama Robben, mchezaji ambaye watahitaji kuwa na huduma yake kwa maana hawafai.
Liverpool imebadili sera zake za usajili na kwamba kwa sasa hawawezi kumsajili mchezaji ambaye baadaye hawatakuwa na fursa na hao kumuuza. Pamoja na uzuri wote wa Robben atakaokuwa nao kwenye soka na kuitikisa duniani, mchezaji huyo ana umri wa miaka 29 na tetesi zilizopo ni kwamba Bayern analipwa zaidi ya pauni 100,000 kwa wiki.
Si mchezaji ambaye ana tatizo la majeraha sana, lakini ukihitaji kumsajili ni lazima atahitaji mkataba wa miaka minne, jambo ambalo litamfanya afikishe umri wa miaka 33 na nusu, huku Liverpool wakiwa na nafasi ndogo sana ya kumbadilisha namba.
Liverpool tayari wamekumbana na matatizo ya wachezaji Andy Carroll na Stewart Downing, hivyo hawatakuwa tayari kurudia kosa kwa mara ya tatu na zaidi ya hilo ni kwamba mchezaji huyo atakuwa ghali kwao.
Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers, anafuata falsafa za soka la Guardiola, kuzingatia zaidi kwenye kupiga pasi, staili ya tiki-taka. Kama Guardiola, baba wa mtindo wa tiki-taka ya kisasa, haoni mahali pa kumpanga Robben, Rodgers ataipata wapi nafasi hiyo? Kwa kipindi chote cha majira haya ya kiangazi, kumekuwa na ripoti za uhamisho wa ajabu sana na wenye kushangaza. Kweli hii ni biashara bomu?

No comments:

Post a Comment