Pages

Thursday, May 30, 2013

YANGA KUACHA WACHEZAJI SABA

KLABU ya Yanga inatarajia kuwatema wachezaji wake saba katika msimu ujao wa ligi kuu na michuano ya kimataifa.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, nyota hao wanatemwa kutokana na kushuka kwa viwango vyao.

Kwa mujibu wa habari hizo, miongoni mwa nyota hao, wamo watakaouzwa kwa mkopo kwa klabu zingine za ligi kuu.

Wachezaji hao ni pamoja na kipa Saidi Mohamed, mabeki Shadrack Nsajigwa, Godfrey Taita, Salum Telela, Ladslaus Mbogo, Stephano Mwasika na kiungo Nurdin Bakari.

Habari hizo zimeeleza kuwa, Mbogo anaachwa kutokana na kuwa mgonjwa kwa muda mrefu na hivyo kushindwa kuitumikia vyema timu hiyo katika ligi ya msimu uliopita.

Tangu alipojiunga na Yanga mwaka juzi, Mbogo ameshafanyiwa operesheni kwa ajili ya kuondoa uvimbe kwenye taya lake.

Wachezaji wanaotarajiwa kuuzwa kwa mkopo ni Nurdin na Saidi kwa vile bado wana mikataba ya kuitumikia Yanga.

Wakati huo huo, klabu ya Yanga imesema inatarajia kuwatangaza nyota wake wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao kabla ya timu hiyo kwenda Sudan.

Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Yanga, Abdalla Bin Kleb alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, wachezaji hao ni wale waliopendekezwa na Kocha Ernie Brandts kutoka Uholanzi.

"Tayari tunayo majina ya wachezaji wapya tuliowasajili kutokana na mapendekezo ya kocha na tunatarajia kuyatangaza wakati wowote wiki ijayo,"alisema.

Bin Kleb alisema kwa sasa wapo katika hatua za mwisho za mazungumzo na baadhi ya wachezaji hao wapya kabla ya kuingia nao mikataba.

Miongoni mwa wachezaji wapya waliosajiliwa na Yanga ni pamoja na mshambuliaji Mrisho Ngasa, aliyekuwa akiichezea Simba kwa mkopo akitokea Azam.

No comments:

Post a Comment