Pages

Wednesday, May 29, 2013

NEYMAR ATAENDELEZA UBABE WA BRAZIL BARCELONA?


BARCELONA, Hispania
KOCHA Mkuu wa Barcelona, Tito Vilanova, anamzungumzia mshambuliaji wake mpya, Neymar na kusema kwamba anaamini hawakuingia kanyaboya kwa mchezaji huyo, alikuwa akiwindwa karibu na klabu zote za Ulaya.

Lakini, mtihani uliopo ni kuona kama Mbrazil huyo ataweza kuendana na soka linalochezwa nchini Hispania.
"Nampongeza mchezaji kwasababu amechagua timu kwa ajili ya sababu za kisoka na si fedha. Ameichagua Barcelona kwasababu anapenda kucheza staili yetu na naamini ataweza kuendana nayo.
"Tumewahi kabla ya klabu nyingine, tunafahamu uwezo wake na pia wametutumia video zake za miaka miwili na nusu iliyopita. Wakati klabu nyingine zilipomfuata, sisi tayari tulishamalizana naye," alisema Vilanova akiwa mwenye furaha kubwa baada ya kuinasa saini ya staa huyo.

Lakini, kuwasili kwa Neymar, lazima kutafungua njia ya ushindani wa namba kwenye kikosi hicho, ambayo tayari wachezaji kama Thiago Alcantara anafikiria kuondoka.
Kutokana na Lionel Messi kuwa ni mtu aliyejihakikishia namba kwenye kikosi hicho, ni wazi kabisa Neymar anaweza kuwa patna wake katika safu yao ya ushambuliaji, jambo litakalowafanya wachezaji kama Cesc Fabregas kusubiri kando.

Kimfumo, Xavi na Andres Iniesta ni wachezaji ambao Tito hatahitaji kuwaweka kando kama tu watakuwa wapo fiti, hivyo Cesc ambaye amekuwa akichezeshwa mbele sasa anaweza akasubiri kitu ambacho kinaweza kumsukuma akaamua kuihama timu hiyo mwisho wa msimu huu, ili kwenda kusaka makali ambapo atapata nafasi ya kucheza muda mwingine.

Lakini, jambo hilo pia litamweka kwenye wakati mgumu kocha Tito, kwasababu kwa kadri unavyokuwa na wachezaji wengi bora, ndivyo unavyokuwa na wakati mgumu wa kupanga kikosi.
Kuhusu Neymar kufanya vyema kwenye kikosi hicho, jambo hilo lina nafasi kubwa hasa ukizingatia historia ya Wabrazil waliowahi kutua kwenye timu hiyo.

Barca ni timu yenye historia ya aina yake kwa wachezaji wa Kibrazil, ambapo mahali hapo yameweza kupita majina makubwa kama Romario, Ronaldo, Rivaldo na Ronaldinho, ambao waliweza kuitawala dunia kutokana na soka lao.
Neymar atakuwa Mbrazil wa 28 kuvaa jezi za wababe hao wa Nou Camp na usajili wake unafungua zama mpya kwa wachezaji wa kutoka nchi hiyo mwenyeji wa Kombe la Dunia 2014.

Mbrazil wa kwanza kusaini kuichezea Barca alikuwa kiungo Fausto dos Santos, ambaye alijiunga na timu hiyo katika msimu wa 1931-1932.
Tangu wakati huo, Wabrazil wamekuwa na alama nzuri katika kikosi hicho, licha ya wengine mara kadha kushindwa kung'ara katika mechi zao za kwanza.

Lakini, ukiwaweka kando wakali kama Alves, Adriano, Belletti na wengineo, wale ambao wametikisa na kubaki kwenye kumbukumbu za wengi ni washambuliaji waliowahi kung'ara mahali hapo.
Kuna orodha ndefu, lakini wababe wao ni pamoja na Evaristo de Macedo, Romario, Ronaldo, Rivaldo na Ronaldinho, ambao hadi leo wanabaki kuwa kwenye historia ya klabu.

Na sasa ametua mshambuliaji mwingine, Neymar. Evaristo alijiunga na miamba hiyo ya Catalan mwaka 1957 na alifunga mabao mengi si pungufu ya 173 kabla ya kuondoka 1962.
Romario yeye alibaki hapo kwa misimu miwili tu, lakini aliweza kutimiza ahadi yake aliyotoa wakati alipotua mahali hapo, kwamba atafunga mabao 30 kwa msimu.

Mwingine aliyefuatia ni Ronaldo, ambaye alisajiliwa katika msimu wa 96-97, alicheza kwa msimu mmoja tu, lakini bado kipindi hicho kilitosha kumfanya kuingia kwenye historia ya Camp Nou. Alifunga mabao 47 katika mechi 51.
Rivaldo alijiunga na timu hiyo mwaka uliofuata akitokea Deportivo na mwaka 1999 kiwango chake cha soka kilimfanya atwaye tuzo ya Ballon d'Or.

Staa wa mwisho wa Brazil kuweka alama zake kwenye klabu hiyo, alikuwa Ronaldinho, ambaye alisajiliwa mwaka 2003 akitokea PSG.
Kiwango chake kiliweza kuibadili timu hiyo ambayo ilikuwa haijatwaa taji lolote kwa misimu mitano na tangu alipotua hapo kila kitu kilibadilika na Barca ikaanza kuwa tishio, ikifanikiwa pia kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

No comments:

Post a Comment