UONGOZI wa Chama cha Soka cha Mkoa wa Lindi (LIREFA),
umelaani vikali vurugu zilizotokea kwenye Uwanja wa Ilulu mkoani humo, wakati
wa pambano la Kariakoo dhidi ya Titanic ya Nachingwea ya Mtwara.
Akizungumza na BINGWA jana Katibu Mkuu wa LIREFA, Luis
Taisamo, alisema pambano la timu hizo
lilivunjika katika dakika ya 67, kutokana na vurugu kubwa zilizosababishwa na
mashabiki wa soka.
Alisema vurugu hizo zinadaiwa kufanywa na baadhi wa
mashabiki wa Titanic, Chama chake kinalaani kitendo hicho kwa nguvu zote, kwa
maelezo kuwa hakiendani na maadili mema ya mchezo wa soka.
Alisema kuwa LIREFA kimesikitishwa na kitendo hicho, kimeona
ni vyema kitoe tamko la kulaani wale wote waliohusika na vurugu hizo, ambazo
zilisababisha usumbufu kwa mashabiki wengine wasio na hatia.
“LIREFA tunalaani vurugu zilizotokea kwenye uwanja wa Ilulu,
ambazo zilisababisha mechi ya fainali uwanjani hapo kuvunjika, pia na
kusababisha usumbufu kwa wengine waliofika kushuhudia pambano,” alisema
Taisamo.
Akifafanua alisema, kamati yake ya Utendaji imeipa Kariakoo
ubingwa wa Mkoa wa Lindi, wakati pambano lilipovunjika ilikuwa mbele kwa mabao
2-0, yaliyofungwa na Nassoro Cholo na Salum Abdil.
No comments:
Post a Comment