Pages

Friday, May 3, 2013

SIMBA KUCHEZA JUMAPILI NA RUVU SHOOTING NA KAMATI YA MASHINDANO KUKUTANA JUMAPILI KUANDAA LIGI YA MABINGWA WA MIKOA


Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inakutana Jumapili (Mei 5 mwaka huu) kupitia maandalizi ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) iliyopangwa kuanza Mei 12 mwaka huu.
Tayari mikoa 18 kati ya 27 kimpira imeshapata mabingwa wao kwa ajili ya RCL itakayotoa timu tatu zitakazopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao (2013/2014).
Kamati hiyo chini ya Uenyekiti wa Blassy Kiondo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF itapokea taarifa ya maandalizi ya ligi hiyo kutoka Idara ya Mashindano ya TFF na kufanya uamuzi juu ya mikoa ambayo haijawasilisha mabingwa wao.
Ligi hiyo itachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini, na ratiba (draw) itapangwa wakati wowote. Ada ya kushiriki ligi hiyo kwa kila klabu ni sh. 100,000 na usajili utakaotumika na ule ule wa ligi ngazi ya mkoa. Hakutakuwa na usajili mpya wa wachezaji.
LALA SALAMA VPL KUENDELEA JUMAPILI
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea Jumapili (Mei 5 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya Ruvu Shooting na Simba itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.15 jioni.
Hiyo itakuwa mechi ya raundi ya 24 kwa timu hizo ambapo Simba iko nafasi ya nne ikiwa na pointi 39 nyuma ya mabingwa Yanga wenye pointi 57, Azam yenye pointi 48 na Kagera Sugar ambayo ina pointi 40. Ruvu Shooting iko katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 31.
Hadi sasa mabao 348 yameshafungwa katika ligi hiyo huku Yanga ikiongoza kwa kufunga 45. Polisi Morogoro yenye pointi 22 katika nafasi ya 12 ndiyo iliyofunga mabao machache ikiwa nayo 13 tu.
African Lyon yenye pointi 19 katika nafasi ya mwisho ndiyo inayoongoza kwa kuwa na kadi nyingi. Timu hiyo inayofundishwa na Charles Otieno ina kadi 44 ambapo kati ya hizo nne ni nyekundu. Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro yenyewe inaongoza kwa kuwa na kadi nyingi nyekundu ambapo hadi sasa inazo saba.

No comments:

Post a Comment