Pages

Friday, May 10, 2013

DRFA YAZIPA TAFU RED COAST, ABAJALO NA FRIENDS RANGERS KWENYE MAANDALIZI YA LIGI YA MABINGWA

Mwenyekiti wa DRFA Almas Kasongo (kushoto) akimkabidhi fedha  Jumanne Ayoub (kulia) ambaye aliwakilisha timu ya Red Coast zawadi ya fedha taslimu 700,000 jana kwenye ofisi za DRFA 

Mwenyekiti wa DRFA Almas Kasongo (kushoto) akimkabidhi fedha Abbas Ngau  (kulia) ambaye aliwakilisha timu ya Abajalo zawadi ya fedha taslimu 600,000 jana kwenye ofisi za DRFA 

Mwenyekiti wa DRFA Almas Kasongo (kushoto) akimkabidhi fedha Shaban Marsila (kulia) ambaye aliwakilisha timu ya Friends Rangers zawadi ya fedha taslimu 500,000 jana kwenye ofisi za DRFA 

Baadhi ya waliohudhuria kikao cha jana

CHAMA cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kimezizawadia timu za Red Coast, Abajalo na Friends Rangers baada ya kuibuka kushika nafasi tatu za juu za Ligi ya Mkoa huo na kufanikiwa kucheza Ligi ya Mabingwa wa mikoa inayotarajiwa kuanza Mei 12 mwaka huu.

Timu hizo zimekabidhiwa fedha taslimu na Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam, Almas Kasongo kwenye ofisi za chama hicho, zilizopo makutano ya mtaa wa Mafia na Bonde, Kariakoo, Ilala.

Mshindi wa kwanza ambaye ni Red Coast walikabidhiwa fedha taslimu 700, 000, huku Abajalo wao wakizawadiwa Sh 600, 000 na Friends Rangers wakijipatia Sh 500, 000.

Akizungumza wakati wa kikao hicho kifupi Mwenyekiti wa DRFA, Almas Kassongo, ambaye ndiye aliyekabidhi fedha hizo kwa wawakilishi wa timu hizo alisema kuwa kiasi cha fedha walichowapa ni kidogo kulingana na mahitaji ya timu kwa sasa ila zitasaidia kuongeza chachu kwenye ushiriki wa Ligi ya Mabingwa.
“Kiasi cha fedha ambacho chama kimetoa tunajua hakikidhi mahitaji yenu ila kitasaidia kuongeza chachu kwenye maandalizi ya Ligi ya Mabingwa wa mikoa”

Timu za Red Coast, Abajalo na Friends Rangers zinawakilisha mkoa wa Dar es Salaam kwenye ligi ya Mabingwa mikoa inayotarajiwa kuanza Mei 12, mwaka huu .

Pia timu uongozi wa DRFA umeahidi kushirikiana nao pia wakawataka wawe wawakilishi wema wa mkoa kwani wadau watapenda kuona moja ya timu hizo zikipata nafasi ya kucheza Ligi daraja la kwanza mwakani.

Wakati huo huo, kamati ya ufundi ya DRFA kesho itakutana na Viongozi wa soka la Wanawake (TWFA), Viongozi wa soka la Vijana na Kamati ya Waamuzi ili kupanga utaratibu wa ligi na pia kuandaa kozi ya makocha kwenye ukumbi wa Harbours Club Kurasini.

No comments:

Post a Comment