Pages

Wednesday, May 29, 2013

CRYSTAL PALACE ITAPONA KWA BUNDUKI ZA AKINA VAN PERSIE, BALE NA SUAREZ?


LONDON, England
CRYSTAL Palace imenyakua tiketi ya kushiriki mikikimikiki ya Ligi Kuu England msimu ujao, baada ya juzi kuinyuka Watford bao 1-0 katika mchezo wa mchujo wa kuwania nafasi hiyo, uliofanyika kwenye Uwanja wa Wembley.

Bao la mkwaju wa penalti iliyofungwa na mshambuliaji Kevin Phillips lilitosha kuipa Palace nafasi ya kufuzu michuano ya Ligi Kuu England msimu ujao. Hilo limekwisha na sasa Palace inasubiri kupambana kwenye ligi.
Kikosi hicho kinachonolewa na Ian Holloway, kinakabiliwa na changamoto nyingi, lakini kubwa ni namna itakavyoweza kupambana na vigogo kwenye ligi hiyo.

Tatizo linalomkabili Holloway ni juu ya wachezaji wake nyota. Wilfried Zaha, atajiunga na Manchester United, mshambuliaji wake nyota Glenn Murray huenda akawa nje ya uwanja hadi Krismasi kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti na mkali wake aliyemfungia bao la ushindi juzi, Kevin Phillips, umri umemtupa mkono, anakaribia miaka 40. 

Kutokana na hilo, kikosi hicho sasa kinasaka sura mpya. Kitu cha kwanza ambacho Holloway anapaswa kukifanya ni kuzungumza na David Moyes kuona kama kuna nafasi yoyote ya Zaha kurejea kwa mkopo kwenye timu yake msimu ujao. 
Zaha amekuwa mchezaji mwenye nguvu na kasi ambayo mara nyingi imekuwa ikiwapa shida mabeki kumzuia na kwamba inapotokea kushindana mbio, kama beki anadhani ataweza kuwahi mpira, atakuwa amejidanganya.

Wachezaji wa aina hii wamekuwa wakiwapa makocha matumaini ya kushinda mechi, kitu ambacho ni wazi Palace itahitaji kwa nguvu zote kuona kinatokea. Tatizo alilonalo Zaha ni moja tu, wakati mwingine huwa haelewi afanye nini wakati anapokuwa na mpira, lakini jambo hilo ni dogo na anaweza kurekebishwa na kocha Moyes na kucheza namna Man United inavyocheza. 

Kinara wao wa mabao, Glenn Murray, alitikisa nyavu mara 31 na kuonyesha kwamba anaweza kufuata nyayo za Rickie Lambert wa Southampton au Grant Holt wa Norwich, ambao walivamia Ligi Kuu kwa kasi yao ya kutikisa nyavu. 
Lakini, mfungaji anapaswa kutayarishwa kwa kipindi kifupi. Pamoja na hilo, kocha Holloway atatakiwa kuendelea kubaki na Kevin Phillips, isimwondoe licha ya kuwa na umri mkubwa.

Phillips ni kama alivyokuwa Teddy Sheringham — alikosa kasi wakati alipokuwa na umri mkubwa, lakini hilo halikuwa tatizo kwake, kwa kuwa alikuwa anajua kufunga. 
Kwa Palace itakuwa kitu kizuri kama wataendelea kuwa na mchezaji huyo mzoefu kwenye kikosi chao kwa sababu pia anastahili zawadi kutokana na kudumu na kikosi hicho kwa muda mrefu.

Aliwahi kuwa kwenye kikosi cha Sunderland na kucheza mechi ya mchujo mwaka 1998; ambapo bao lake alilofunga liliifanya Sunderland kuongoza kwa 2-1 dhidi ya Charlton katika mechi ambayo ilimalizika kwa sare ya 4-4, baada ya dakika za nyongeza — lakini baadaye alitolewa na kisha timu yake, Sunderland kufungwa kwa penalti 7-6.

Mwaka 2007, mabao yake matatu kwenye nusu fainali yaliifanya West Bromwich Albion kucheza Wembley — lakini mabeki wa Derby walimtoa nje kwenye mechi ya fainali na Albion ilishindwa kufuzu.
Mwaka 2011, alianzishwa upande wa Blackpool kwenye mechi dhidi ya West Ham, lakini bao la Ricardo Vaz Te la dakika 87 liliipa Hammers ushindi wa 2-1 na hivyo kukwea Ligi Kuu.

Lakini, kwa sasa Palace wapo njia panda. Kwanza, wanataka kulinda fedha zao, kuzitumia kuendeleza Selhurst Park na kujihakikishia ulinzi wa klabu kwa siku za baadaye.
Kinachowaweka njia panda ni juu ya kama wafanye usajili wa nguvu kwa ajili ya msimu ujao. Lakini, pia kutumia fedha nyingi kwenye usajili, jambo hilo nalo ni hatari.

Kingine, Holloway ni lazima aamue moja, kama kucheza soka la kufungua zaidi, mtindo ambao umepata mashabiki wengi sana Blackpool. Hawaruhusu kufungwa mabao mengi kama timu inavyocheza kwa sasa, lakini Holloway ni wazi atahitaji kucheza soka la kuvutia.
Holloway roho yake itamtulia kutokana na kipa wake, Julian Speroni - kwa kuwa Palace chini yake ipo kwenye mikono salama. Na hata mabeki wake wanaomlinda nao wapo vizuri.

Danny Gabbidon amekuwa akicheza vizuri msimu huu, lakini ikumbukwe alipata shida sana walipomenyana na West Ham na QPR kwenye Ligi Kuu. Na sasa amefika kwenye ligi hiyo na atakwenda kukumbana na washambuliaji kama Luis Suarez, Robin van Persie na Gareth Bale. 
Kwenye safu ya kiungo, Palace inahitaji kuwa na kasi kubwa. Mile Jedinak alicheza vizuri na Stuart O’Keefe alikuwa mwenye kujiamini, lakini kwenye Ligi Kuu unahitaji kuwa na viungo wajanja wajanja ndani ya uwanja.

Palace ina wachezaji wake wawili ambao wanaweza kuwa tishio kwenye ligi hiyo. Yannick Bolasie hakuwa mwenye bahati katika mchezo huo wa juzi kutokana na kuwekwa benchi, wakati Jonathan Williams amekuwa mchezaji anayefukuziwa na klabu nyingine na hilo linatokana na kwamba yeye ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa.

No comments:

Post a Comment