Pages

Tuesday, April 23, 2013

SAMIR NASIR AGEUKA LULU DAKIKA ZA MWISHO



ALIPOJIUNGA na Manchester City ni wazi kwamba alionekana lulu, na kilichomchosha zaidi kukaa kwa washika Bunduki wa jiji la London ni kukaa misimu mingi bila kutwaa taji lolote. Samir Nasir alitaka kufanya kazi ambao licha ya kumpa mshahara mzuri lakini pia imlipe kwa maana ya mafanikio kwa timu anayoichezea.

Kocha wa Manchester City, Roberto Mancini alijiona amefanya uamuzi sahihi kwa kumanasa kiungo mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kufunga mabao. Alisaidia kuipa ubingwa timu hiyo msimu uliopita na kujivuna kuwa katika kikosi cha mabingwa wa Uingereza.

Kwa msimu huu, hakuonekana kuwa ni mwenye makali, hasa baada ya City kumnyakua Yaya Toure ambaye amekuwa chaguo la kwanza kwa Mancini huku Nasri akipewa nafasi chache za kucheza na mara nyingi alikuwa hatoi mchango uliotarajiwa na Mancini.
Alionyesha kuwa si mwenye furaha ndani ya kikosi cha City msimu huu, hasa kutokana na kusugua benchi kwa muda mrefu na wakati mwingine kusumbuliwa na majeraha ambayo kwa ujumla yalimfanya ashindwe kabisa kuwika.

Katika moja ya mechi kocha Mancini alilumbana na Nasri hasa kwa kumtuhumu kushindwa kufuata maelekezo yake hii ilitafsiriwa kwamba siku za kijana huyo Mfaransa kwenye kikosi cha City zimekwisha kwani kulifutiwa uvumi mkali juu ya nyota huyo kutaka kuondoka  katika msimu wa dirisha dogo.
Sababu ya kutaka kuondoka aliiweka wazi kwa kusema kwamba kiwango chake kimeonekana kutokumfurahisha kocha wake hivyo yawezekana kuna klabu ikaona anafaa kuitumikia . “Mancini aliniambia kwamba haridhiki na kiwango changu, katika mazingira haya ni lazima ujitume sana mazoezini, lakini kama hafurahi basi jambo la muhimu ni kuondoka,” alisema.

Kocha Mancini alisema anataka kumtimua na alimtoa kwenye kikosi mara baada ya kupishana kauli  na hakumpanga katika mechi tano mfululizo bila sababu wala kumueleza chochote. “Ni kweli sijawa na msimu mzuri, lakini si kweli kwamba nimeshuka kiwango changu kwa asilimia 50, unapokuwa hupewi nafasi na kuaminiwa mara kadhaa kila unachofanya hata kama ni kizuri hakionekani,” alisema.

Lakini nini alichotakiwa kufanya Nasri? Anachofanya sasa kwa timu yake pengine ndiyo jambo ambalo alitakiwa kufanya tangu mwanzo wa msimu hasa kutokana na ukweli kwamba kwa sasa amekuwa mtu anayetoa mchango muhimu sana kwa timu yake akicheza katika nafasi ya kiungo mshambuliaji.
Kosa moja alilokuwa akilifanya Mancini ingawa hakutaka kukubali ni kumpanga Nasri katika nafasi ya kiungo mchezeshaji huku akimpa jukumu la kuwalisha mipira washambuliaji na kusaidia safu ya ulinzi, na wakati huo akitaka kuona matunda yake katika kufunga mabao.
Wanaomtazama sasa Nasri watamuona kwamba amerejea katika kiwango chake, hii inatokana na ukweli kwamba amekuwa akipangwa katika nafasi sahihi ambayo inamfanya awe na uwezo wa kufanya mambo yake kwa uhuru zaidi kuliko ilivyokuwa mwanzo.

“Inatakiwa kufahamu aina ya mchezaji na aina ya uchezaji wake, Mancini hakuwa akimtumia vizuri Nasri, na iliniuma alipomsuhutumu kwamba ameshuka kiwango, kiuhalisia Nasri ni kiungo mshambuliaji kumbadilisha namba ni sawa lakini unapombadili usitegemee kupata matunda kama yaleyale ya mwanzo,” anasema kocha wake wa zamani Arsene Wenger.

Wenger anaongeza kwa kusema kuwa, alipomsajili, alimsaidia katika kubadili uchezaji wake kutoka ule wa taratibu na kuwa wa kasi, na alimjengea mazingira mazuri ya kuwa na maamuzi pale anapokuwa na nafasi, lakini kwa Mancini alimhitaji Nasri kuchezesha wenzake na hata akifunga bao basi itokee kama dharura.
Kwa sasa Nasri ameoenekana kuwa lulu kwa City, mchango wake umeiwezesha timu hiyo kuingia fainali ya kombe la FA baada ya kuitoa Chelsea lakini pia amekuwa akimianiwa kuwa katika kikosi cha kwanza cha vijana wa Etihad.

No comments:

Post a Comment