Pages

Thursday, February 14, 2013

SIMBA WATAMBA KUISAMBARATISHA LIBOLO JUMAPILI

MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage ametamba kuwa, kikosi chake kinao uwezo wa kutoa kipigo kwa wapinzani wao,Libolo ya Angola katika mchezo wa michuano ya klabu bingwa Afrika.

Rage amesema kwa kawaida, Simba huwa inabadilika inapocheza katika michuano ya kimataifa hivyo amewataka mashabiki wa timu hiyo wasiwe na wasiwasi kuhusu mechi hiyo.

Simba na Libolo zinatarajiwa kumenyana Jumapili katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye mjini Luanda.

Akizungumza mjini Dar es Salaam, Rage alisema mabadiliko ya benchi la ufundi hayawezi kuiathiri Simba katika mechi hiyo kwa vile vijana wake wana ari kubwa ya kuonyesha maajabu.

"Ni kweli baada ya kumuondoa Milovan Cirkovic mfumo wa uchezaji umebadilika, lakini tumejipanga vyema kushinda mechi hiyo na sababu ya kufanya hivyo tunayo,"alisema.

Rage alisema wachezaji wote wapo katika hali nzuri na timu inatarajiwa kurejea Dar es Salaam kutoka Arusha, ambako ilikuwa imeweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo.

Wakati huo huo, kiingilio cha chini katika mechi kati ya Simba na Libolo kitakuwa sh. 5,000

Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, viingilio vingine vitakuwa sh. 10,000 kwa jukwaa la VIP C, sh. 15,000 VIP B na sh.30,000 VIP A.

Kamwaga alisema maandalizi kwa ajili ya mechi hiyo yanakwenda vizuri na tiketi zinatarajiwa kuanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo.

No comments:

Post a Comment