Wachezaji wa Burkina Faso wakishangilia
Wachezaji wa Nigeria wakishangilia
JO’BURG, Afrika Kusini
Nigeria na Burkina Faso zote zilipangwa kundi la C,
ambapo mechi ya makundi baina yao
iliisha kwa sare ya 1-1, Super Eagle ikitangulia kufunga dakika ya 23 kupitia
Emmanuel Emenike, kabla ya Burkina kuchomoa dakika ya 90 kupitia Alain Traore
MICHUANO ya 29 ya Kombe la Mataifa Afrika, inahitimishwa leo
kwenye dimba la Soccer City jijini hapa, ambapo Tai wa Nigeria watakapojaribu kuizuia Burikina Faso
kufanya kile ilichofanya Zambia
katika fainali ya mwaka jana dhidi ya Ivory Coast.
Nigeria
inaumana na Burkina Faso leo katika fainali kali, inayofanana na ya mwaka jana,
ambapo timu iliyokuwa ikipewa nafasi ya kutwaa ubingwa (Ivory Coast) iliumbuka na kulala kwa mikwaju ya
penati dhidi ya timu iliyokuwa ikidharauliwa (Zambia).
Tofauti na mwaka jana ambapo bingwa alipatikana baada ya
dakika 120, kwa mikwaju ya penati, wachambuzi wa soka hawatoi alama nyingi za
ubashiri juu ya marejeo ya kupata bingwa kwa changamoto hiyo katika fainali ya
leo.
Nigeria inapewa
nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa tatu wa fainali hizi, baada ya kufanya hivyo
katika miaka ya 1980 na 1994, licha ya ukweli kuwa hiyo ni fainali yao ya kwanza tangu 2000 walipokubali kichapo mbele ya
‘Simba Wasioshindika’ Cameroon.
Hata hivyo, Burkina Faso
‘Les Etalons’ haina cha kupoteza katika fainali yao
hii ya kwanza ya AFCON, ingawa hiyo haitajwi kuwa sababu itakayowafanya
wasipiganie ubingwa hadi tone la mwisho la jasho, ili kuimarisha rekodi yao mashindanoni.
Mafanikio pekee kwa Burkina Faso katika fainali hizi
kuishia nusu fainali tu mwaka 1998 ilipokuwa mwenyeji wa mashindano ya mwaka
huo.
Zilikotokea: Nigeria na Burkina
Faso zilitokea katika kundi la C, ambalo walipoumana
katika mechi baina yao
walitoka kwa sare ya 1-1, Super Eagle ikitangulia kufunga dakika ya 23 kupitia
Emmanuel Emenike, kabla ya Burkina kuchomoa dakika ya 90 kupitia Alain Traore.
Emenike ambaye ni kianara wa mabao akiwa na mabao 4 hadi sasa,
atakuwa sehemu ya kikosi cha Nigeria,
huku Traore wa Burkina mwenye mabao matatu akiwa majeruhi, ingawa nafasi yake
inajazwa vema na Jonathan Pitroipa – aliyefutiwa kadi nyekundu.
Katika robo fainali ya michuano hii, Burkina Faso iliishangaza Togo kwa bao 1-0 katika pambano la dakika 120,
kabla ya kuing’oa Ghana kwa
matuta katika nusu fainali – baada ya sare ya bao 1-1 ya dakika 120 za pambano hilo lililoharibiwa na
mwamuzi Slim Jdidi.
Kwa upande wao Nigeria
katika robo fainali walivuna ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya timu iliyokuwa
ikipewa nafasi kubwa ya kufika fainali ya Ivory Coast, kisha ikaja kushinda
nusu fainali kwa ushindi wa kishindo wa mabao 4-1 dhidi ya Mali.
Nyota wa kuchungwa,
Nigeria: John Obi Mikel – Kiungo
huyu wa Chelsea na mteule anayewania tuzo ya
Mchezaji Bora wa Mashindano, amekuwa na fainali za kuvutia, akiwa mhimili wa
soka la kitabuni katika idara ya kiungo, alikoiwezesha Nigeria kucheza ikiwa huru na
kuzalisha mashambulizi kutokea kati.
Burkina Faso: Jonathan Pitroipa – Nusu fainali tata
kwa upande wake, aliyonyimwa penati na kujikuta akiambulia kadi na kutolewea
nje ya dimba, inaweza kuwa chachu ya kusafishwa kwake na kurejeshwa mchezoni
leo baada ya kufutiwa adhabu.
Bao pekee katika robo fainali, mchango uliotukuka katika
nusu fainali na kukosekana kwa nyota mwenzake wa ‘Les Etalons’ na mpachika
mabao tegemeo wa kikosi hicho, majeruhi Alain Traoré, kunamfanya Pitroipa kuwa
‘mtu hatari’ wa kikosi cha Burkina.
No comments:
Post a Comment