Maandalizi mazuri, uwekezaji mkubwa wa miundombinu
na utaalam na usajili mzuri yameipatia Azam FC ushindi mnono kwa kuifunga Mtibwa
Sugar 4-1 katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom uliochezwa kwenye Uwanja wa
Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
Ushindi huo wa ugenini umeiongezea Azam FC pointi
tatu na kufikisha jumla ya pointi 33 ikiwa sawa na Yanga wakitofautiana kwa
magoli, na Simba kuwa ya tatu ikiwa na pointi 27.
Katika mchezo huo ujio mpya wa mchezaji Kipre
Tchetche pamoja na kandanda safi lililochezwa na Azam FC limeipatia ushindi timu
hiyo na kuongeza rekodi ya kuifunga timu Mtibwa kwa mara ya nne ikiwa katika
uwanja wa nyumbani kwao Manungu.
Azam FC walianza mchezo huo wakijiamini na mapema
katika dakika ya 14 mchezaji Jockins Atudo aliipatia Azam FC goli la kwanza
akimalizia krosi iliyopigwa na Abdi Kassim ‘Babi’.
Dakika ya 21 Vincent Barnabas akaisawazishia Mtibwa
Sugar kwa mpira wa kichwa baada ya kuteleza kwa kipa Mwadini Ally wakati akitaka
kudaka mpira aliorudishiwa kwa kichwa na beki Jockins Atudo, timu zikaenda
mapumziko zikiwa sare ya 1-1.
Kipindi cha pili kilikuwa cha Azam FC, walipata goli
la pili dakika 47 lililofungwa na mshambuliaji Brian Umony aliyecheza vizuri na
Humphrey Mieno na kuwapoteza mabeki wa Mtibwa na kuandika goli hilo ambalo
lilibadili matokeo yakawa 2-1.
Azam FC walifanya mabadiliko dk 45 alitoka Himid Mao
akaingia Ibrahim Mwaipopo alieyefanya kazi nzuri kipindi cha kwanza, dk 60 Abdi
Kassim alipumzishwa baada ya kuitendea haki safu yake ya ushambiliaj nafasi yake
ikachukuliwa na Tchetche Kipre na dk 75 alitoka Brian Umony aliyefunga goli la
pili akaingia kiungo Jabir Aziz.
Mabadiliko hayo yaliimarisha kikosi cha Azam FC na
kuzidi kuitesa Mtibwa Sugar ambao walionekana kupata tabu, dk 88 Kipre Tchetche
aliipatia Azam FC goli la tatu kwa shuti akimalizia mpira aliotengewa na
Humphrey Mieno na kupeleka matokeo kuwa 3-1.
Mshambuliaji huyo (Kipre) kutoka Ivory Coast
alitumia vizuri dakika za nyongeza kwa kuipatia Azam FC goli la nne na
kuhitimisha karamu ya magoli baada ya kuunganisha vizuri mpira uliopigwa na
nahodha Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na kumaliza mchezo Azam FC ikiondoka na
ushindi wa 4-1 dhidi ya wenyeji wao Mtibwa Sugar.
Azam FC ilianza safari ya kurejea jijini Dar es
Salaam mara baada ya mchezo huo kwa ajili ya kuanza maandalizi kwa ajili ya
mchezo wao wa kwanza wa kimataifa katika mashindano ya Kombe la Shirikisho
Afrika dhidi ya Al Nasri Juba ya Sudan Kusini utakaochezwa wiki ijayo jijini Dar
es Salaam.
Kikosi cha Azam FC kilichofanya mauaji kiliundwa na
Mwadini Ally, Himid Mao/Ibrahim Mwaipopo 45’, Malika Ndeule, Jockins Atudo,
David Mwantika, Michael Bolou, Brian Umony/Jabir Aziz 75’, Salum Abubakar ‘Sure
Boy’ (cpt), Abdi Kassim ‘Babi’/Tchetche Kipre 60’ Humprey Mieno na Khamis
Mcha
No comments:
Post a Comment