Pages

Monday, January 7, 2013

SIMBA YAJITOA MAPINDUZI LICHA YA KUFUZU KWA HATUA YA NUSU FAINALI

Kiungo wa Simba SC, Abdallah Seseme akijaribu kumzuia kiungo wa Bandari ya Zanzibar kwenye mchezo wa Kombe la Mapinduzi, kundi A uliochezwa jana usiku  kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, timu hizo zilitoka sare 1-1.

LICHA ya  kufuzu hatua ya Nusu Fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi jana, Simba SC italazimika kuiachia timu yao ya pili, maarufu kama Simba B iendelee na michuano hiyo kwa sababu kikosi cha kwanza kitaondoka nchini kesho kutwa kwenda Oman.

Kocha Mkuu wa Simba SC, Mfaransa Patrick Liewig amesema  kwamba, anataka kwenda Oman na kikosi kamili ili aweze kuwajua wachezaji wote na kuweza kuipanga vyema timu yake.

Simba jana ilifuzu Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi, baada ya kutoka sare ya 1-1 na Bandari ya Zanzibar kwenye mchezo wa mwisho wa Kundi A, uliochezwa uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1, ambapo  Bandari wakitangulia kupata bao kwa penalti, mfungaji akiwa Haitham Juma dakika ya sita kabla ya Kiggi Makassy kuisawazishia Simba SC dakika ya 16.

Refa alitoa penalti kwa Bandari baada ya Haruna Shamte kumchezea rafu Fauzi Ally katika eneo la hatari na Haitham akaenda kupiga penalti, ambayo ilipanguliwa na kipa Dhaira na mpira kumkuta tena mpigaji, aliyeukwamisha mpira nyavuni.

Kiggi alifunga bao kwa mpira wa adhabu kutoka upande wa kulia wa uwanja, baada ya Abdallah Seseme kuangushwa.   
Kipindi cha pili, Simba walianza kwa kuimarisha kikosi chao wakiwaingiza kwa mpigo, Mwinyi Kazimoto, Haruna Chanongo na Jonas Mkude kuchukua nafasi za Mussa Mude, Salim Kinje na Ramadhani Singano ‘Messi’, wakati Bandari walimtoa kipa wao Hassan Hajji na kumuingiza Ahmad Suleiman.

Kwa matokeo hayo, Simba SC imeungana na Tusker ya Kenya kufuzu Nusu Fainali ya michuano hiyo huku Tusker ikiwa kinara wa kundi kwa pointi zake saba na Simba imeingia kama mshindi wa pili kwa pointi zake tano.

Simba inatarajia kuondoka na wachezaji wake wote hata walioitwa kwenye timu ya taifa kwani kocha anahitaji kukaa na kuwajua wachezaji hivyo uongozi wa Simba upo kwenye mazungumzo na shirikisho la Soka nchini ili wachezaji walioitwa kwenye timu ya taifa waruhusiwe kuungana na timu kwenye safari ya Oman 

Wachezaji wa Simba SC walioitwa Stars ni kipa Juma Kaseja, mabeki Amir Maftah na Shomari Kapombe, viungo Amri Kiemba na Mwinyi Kazimoto na mshambuliaji Mrisho Ngasa.
Katika wachezaji wote hao walioitwa Stars, walio kwenye kikosi cha Simba kinachocheza Kombe la Mapinduzi ni Kapombe na Mwinyi Kazimoto pekee. Kaseja, Ngassa, Kiemba ni majeruhi, wakati Amir Maftah imeelezwa ana madai yake anayosubiri alipwe ndipo ajiunge na timu. 

No comments:

Post a Comment