KOCHA wa Arsenal, Arsene
Wenger amedai kwamba klabu yake bado inanafasi ya kushinda taji la Ligi Kuu ya
England msimu huu, licha ya kuwa pointi 11 nyuma ya vinara wa ligi hiyo
Manchester United, baada ya kutoa sare ya mabao 3-3 dhidi ya Fulham, Jumamosi.
Baada ya matokeo mabovu
kwenye wiki za karibuni, Wenger anaamini kwamba kikosi chake kinakuwa kila siku
na kinaweza kupambana kuwania taji hilo kubwa zaidi kwenye soka la England,
Arsenal kwa sasa wanakamata nafasi ya nane kwenye ligi wakiwa na matokeo mabovu
kila kukicha.
Wenger ameendelea
kuamini kwamba timu yake inaweza kufanya vizuri msimu huu, licha ya Gunners kushinda
mechi moja tu kati ya nne za mwisho, huku beki yao ikiruhusu mabao 14 katika
mechi nne za mwisho pekee.
Alipoulizwa kama timu
yake inaweza kuibuka na kutoa upinzani kwenye ligi wakati wa mzunguko wa pili
wa ligi hiyo, Wenger alijibu. “Ndiyo, kwanini ishindikane,” Wenger alijbu kwa
hasira akionekana kukerwa na swali hilo.
“Tumetoka kucheza mechi
tatu ngumu, hasa mbili za kwanza,” akimaanisha kichapo cha 2-1 kutoka kwa Man United
na sare ya 2-2 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Schalke. “Tulilazimika kuinuka
baada ya mechi ya United (Man) na tukaenda Ujerumani kujitoa mpaka mwisho.
Wenger alisema kwamba
watu wote kwenye timu wamesikitishwa na matokeo ya mechi ya Fulham kwa sababu
timu ilitengeneza nafasi nyingi na kushindwa kuzitumia na hatimaye wakajikuta
wanapata sare, lakini alisema kuna mengi mazuri ambayo aliyaona kwenye mechi
hiyo na kudai kwamba timu ilicheza vizuri sana kitu kilichamfanya aendelee
kuiamini timu hiyo.
Kitu kikubwa ambacho
kilimfurahisha Wenger kwenye mechi hiyo ni kiwango kilichoonyeshwa na
mshambuliaji Olivier Giroud ambaye alifunga mabao mawili kwenye mechi hiyo.
No comments:
Post a Comment