Pages

Saturday, October 6, 2012

WAAMUZI WATATU WAONDOLEWA, SIMBA YAPIGWA FAINI

Mwamuzi Mathew Akrama (mpira uko chini ya miguu yake) aliyeondolewa

Kamati ya Ligi imewaondoa waamuzi watatu wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa kushindwa kumudu michezo waliyopangiwa. Waamuzi hao ni Mathew Akrama wa Mwanza aliyechezesha mechi namba 80 ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Simba iliyochezwa Oktoba 3 mwaka huu.
 
Wengine ni Paul Soleji wa Mwanza aliyechezesha mechi kati ya Simba na Tanzania Prisons, na mwamuzi msaidizi namba mbili kwenye mechi hiyo Mwarabu Mumbi wa Morogoro. Pia mwamuzi msaidizi namba mbili wa mechi ya Yanga na Simba, Ephrony Ndissa wa Dar es Salaam amepewa onyo.
 
Kamishna wa mechi namba 28 kati ya Yanga na African Lyon, Pius Mashera ameondolewa kwenye orodha ya makamishna wa ligi hiyo kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (Pre match meeting) na uwanjani.
 
Vilevile Mashera kwenye ripoti yake aliwasilisha malalamiko dhidi ya msimamizi wa kituo cha Dar es Salaam, na kwa vile suala hilo ni la kinidhamu ametakiwa alipeleke kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF.
 
Nayo Simba imepigwa faini ya jumla ya sh. 600,000 kwa kuchelewa kufika kwenye pre match meeting ya mchezo wao dhidi Tanzania Prisons (sh. 100,000) na kwa washabiki wake kuwatupia chupa za maji waamuzi wa mechi hiyo (500,000).
 
Pia Kamati ya Ligi imeagiza kuwa kwa vile suala la kipa Shabani Kado wa Mtibwa Sugar kudaiwa kumpiga kiongozi mmoja wa Ruvu Shooting mara baada ya mechi kati ya timu hizo iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex ni la kinidhamu lipelekwe kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF.
 
YANGA, AFRICAN LYON KUTOVAA BEJI YA MDHAMINI
Kwa vile msimu huu mdhamini mwenyewe ndiye anayegawa vifaa kwa timu, Kamati ya Ligi imeagiza Vodacom iandikiwe barua na nakala kwa klabu zote ili kujua timu ambazo tayari zimekabidhiwa vifaa hivyo zikiwemo logo na siku ambapo timu husika zilipokea.
 
Baada ya majibu ya Vodacom ndipo Kanuni za Ligi Kuu zitakapotumika kutoka adhabu kwa timu ambazo zitabainika kuwa zilipokea vifaa lakini hazikuvitumia.
 
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment