Pages

Wednesday, September 19, 2012

KLABU LIGI KUU, WADHAMINI VODACOM KUTETA


Klabu za Ligi Kuu ya Vodacom zimekubaliana kukutana na mdhamini (kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom) kuzungumzia kipengele cha mkataba wa ligi hiyo kinachozuia kampuni nyingine za mawasiliano kudhamini timu zinazocheza Ligi Kuu.
 
Maazimio hayo yalifikiwa jana (Septemba 18 mwaka huu) katika kikao kati ya klabu hizo na Kamati ya Ligi kilichofanyika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo Wallace Karia.
 
Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura.
 
Maazimio mengine ya kikao hicho ni TFF kuiandikia barua African Lyon ambayo itaipeleka kwa mdhamini wake (Zantel) ikielezea hatua hiyo ili kusimamisha udhamini huo wakati ikisubiri matokeo ya mazungumzo kati ya klabu hizo na mdhamini wa Ligi Kuu juu ya kipengele cha kuzuia washindani wa Vodacom.
 
Katika mkutano huo, watendaji wawili wa Kamati ya Ligi ambayo iko katika kipindi cha mpito kuelekea kuundwa kwa Bodi ya Ligi walitambulishwa kwa klabu hizo. Watendaji hao ni Silas Mwakibinga ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) na Joel Balisidya ambaye ni Ofisa wa Ligi (LO).
 
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment