Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Monday, May 9, 2016

SERENGETI BOYS YATAKIWA KURUDI NA KOMBEMWENYEKITI wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Dioniz Malinzi amewataka wachezaji wa timu ya soka ya vijana wa Tanzania wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kwenda kupambana na kurudi na kombe.
 Malinzi aliyasema hayo kwenye hafla ya kukabidhi bendera ya taifa kwa timu inayokwenda Goa, India kushiriki mashindano maalumu ya soka ya kimataifa kwa vijana (AIFF Youth Cup 2016 U-16) yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka nchini humo (AIFF), iliyofanyika kwenye Uwanja wa Karume, zilipo ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
Kabla ya kuanza kutoa nasaha Malinzi alisema, Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amemtuma kuwapa salamu wachezaji hao kuwa amefurahi timu hio kupata nafasi ya kwenda kwenye mashindano hayo, hivyo wafahamu wanakwenda kupambana kwa ajili ya watanzania.
“Ninafahamu timu hii inafundishwa na kocha mwenye uzoefu na Kim Poulsen hivyo watafanya vizuri kwenye mashindano hayo hivyo mkapambane ili mwisho wa siku mrudi na kikombe”, alisema Malinzi
Naye balozi wa India hapa nchini, Sandeep  Arya aliwaambia wachezaji hao kuwa wamealikwa kwenye mashindano kwa vile Tanzania inaonekana kuwa na vipaji na kuwataka kwenda kuonesha ushindani wa kweli.
Nahodha wa timu hiyo, Issa Abdi aliwaomba watanzania kuwaombea kwani wanaamini wanakwenda kuwakilisha watanzania na Afrika kwa ujumla kwani ni timu pekee inayotoka Afrika na watahakikisha wanarudi na ushindi.
Serengeti boys inatarajia kuondoka nchini jumatano  kwenda India kushiriki michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Mei 12 na watafungua dimba na vijana wenzao wa timu ya Marekani.
Mbali ya washiriki wenyeji ambao ni India, timu za taifa za vijana kutoka nchi za Marekani, Korea Kusini, Malaysia na Tanzania zitashiriki michuano hiyo ambapo michezo itachezwa kwa mfumo wa ligi kwa kila timu kucheza michezo minne.
 AIFF kimeandaa mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi chao kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana zitakazofanyika nchini humo mwaka 2017.